Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto amesema lugha anayotumia mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump ndiyo iliyotumiwa na madikteta Adolf Hitler na Benito Mussolini.
Amesema hayo kwenye mahojiano na gazeti la Excelsior ambayo yamechapishwa kwenye gazeti hilo Jumatatu.
Kiongozi huyo amesema matamshi ya Trump yameathiri uhusiano kati ya Mexico na Marekani, kwa mujibu wa shirika la habari la AP.
Alipoulizwa kuhusu Trump, Pena Nieto alisema mambo ambayo mgombea huyo amekuwa akiyafanya na kuyapendekeza “yamewahi kusababisha maafa makubwa katika historia.”
“Hivyo ndiyo Mussolini alijitokeza na ndivyo Hitler alivyojitokeza,” amesema Pena Nieto.
Bw Pena Nieto alikuwa hajazungumza moja kwa moja kumhusu Bw Trump ambaye ameahidi kujenga ua kati ya Mexico na Marekani ili kuzuia wahamiaji kutoka nchi hiyo wasiingie Marekani.
Bw Trump alisema wahamiaji hao huingiza mihadarati na uhalifu Marekani na kwamba ni “wabakaji”.
Mfanyabiashara huyo kutoka New York amekuwa akiongoza kwenye kura za maoni kati ya wale wanaowania kueperusha bendera ya chama cha Republican kwenye uchaguzi mkuu Novemba na viongozi wa sasa na wa zamani wa Mexico wameanza kueleza wasiwasi wao.
Marais wa zamani Vicente Fox na Felipe Calderon pia wamemtaja Hitler wakimzungumzia Trump.
Bw Pena Nieto amesema kamwe Mexico haitafadhili mpango wa kujenga ukuta mpakani kama alivyopendekeza Bw Trump.
Lakini ameeleza matumaini kwamba wapiga kura watamkataa Bw Trump.