Donald Trump ni Zaidi ya Mgombea Urais wa Marekani Msema Ovyo

Mtia nia ya urais wa Marekani kupitia tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump ameelezewa kuwa tishio kwa wapanga sera za Marekani wajulikanao kama “the stablishment.”

Marekani kuna genge la watu mashuhuri wa aina mbalimbali wanaoshika hatamu za Taifa hilo kubwa duniani wajumuisha wanachama wa vyama vikuu viwili vya nchi hiyo Democrats na Republican.

Genge hilo lenye azma ya kuitawala dunia kupitia kile kiitwacho mfumo mpya wa ulimwengu au ‘New World Order’, huendeshwa na genge jingine dogo lijulikana kama “The Globalists.”

Watu hawa hujumuisha wamiliki wa mabenki makubwa, wamiliki wa viwanda vikubwa vikiwamo vile vya silaha, kampuni kubwa, wanasiasa na wamiliki na waandamizi wa vyombo vya habari.

Genge hilo limeunda mashirika maalum kutekeleza ajenda yao ya kuitawala dunia chini ya serikali moja, sarafu moja, jeshi moja na mfumo mmoja wa siasa.

Mashirika hayo ni pamoja na The Council on Foreign Relations (CFR) lililoundwa mwaka 1920. Tangu CFR iundwe, hakuna rais hata mmoja wa Marekani ambaye ametoka nje ya shirika hili.

Shirika jingine ni lile liitwalo The Bilderberg Group au kifupi Bilderberg. Hili ni jukwaa maalumu la kuandaa wanasiasa watarajiwa kuongoza nchi mbalimbali za Ulaya na Marekani.

Trialateral Commison ni shirika jingine la kistratejia zaidi ambalo huhakikisha kuwa nchi za Ulaya, Marekani na Japan zinaoanisha mambo yao ili kuendelea kutawala dunia.

Watu wa ndani na wa nje

Watu wote wanaoshiriki siasa za Marekani wamegawika katika makundi mawili makuu- moja linaitwa Insiders yaani watu wa ndani ya mfumo nilioeleza na jingine Outsiders yaani watu walio nje ya mfumo hupo.

Kati ya wagombea wote wanaowania urais wa Marekani, ni Donald Trump ndiye anayeonekana kuwa mtu kutoka nje ya mfumo nilioueleza hapo juu kwa sababu yeye hayupo CFR, Bilderberg wala Trilateral.

Kwa siasa za Marekani, Donald Trump ni mtu wa nje hivyo hata kama ni mwanachama wa Chama cha Republican na anashinda katika kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa mgombea urais wa chama cha Republican bado haaminiki na washika dau wakuu wa chama hicho.

Kwa jinsi mfumo wa siasa za Marekani ulivyo, mtu anayestahiki kubeba jukumu la kuwa mgombea urais iwe ni kwa Chama cha Republican au Democrats lazima utokane na mfumo niliouelezea hapo juu.

Sababu ni kwamba mtu anayetokana na mfumo huo anajua malengo ya muda mrefu ya genge linalotawala Marekani hivyo akiwa rais hatokwenda kinyume na matakwa ya genge hilo.

Mtu kama Donald Trump, bilionea wa majumba ya kamari (casinos) na wa majumba ya kupanga (real estate) nchini Marekani, kwa kuwa ni mtu wa nje ya mfumo hivyo haaminiki kuliongoza taifa hilo kwani akifanikiwa kuwa rais atafanya uamuzi ambao utaliathiri genge hilo.

Ni kweli Trump anatishia masilahi ya wakubwa?

Kwa mujibu wa jarida maarufu Marekani la Wall Street Journal na vyombo vingine vya habari nchini humo, kauli za Donald Trump zinaelezewa kuwatia hofu matajiri wa Marekani kwamba akishinda urais atafanya mageuzi ya sera mbalimbali zilizokuwa zinawanufaisha wao.

Miongoni mwa kauli hizo ni ile ya kupinga mikataba ya kibishara inayofuta kodi ya ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini Marekani, mikataba ambayo inawanufaisha wafanyabiashara wakubwa na wenye viwanda.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, chini ya kichwa cha habari “As Stock Market Plunges, Donald Trump Takes a Worldview”, Trump anaelezewa kuwanyima usingizi wafanyabiashara na wenye viwanda wanaonufaika na mikataba hiyo.

Katika makala hiyo gazeti hilo liliandika “Mr. Trump has said that bad trade deals with China and Mexico are to blame for a sluggish American economy and weak job creation.

Kwamba Trump amesema mikataba mibaya ya kibiashara na China na Mexico ndiyo sababu ya kuzorota uchumi wa Marekani na uzalishaji dhaifu wa fursa za ajira.

Ameahidi kufanya mikataba bora na nchi nyingine kulinda wafanyakazi wa Marekani na ametishia kupandisha kodi kwa bidhaa kutoka nje zinazoingizwa Marekani ili kuinua uzalishaji wa ndani.

Mikataba inayotajwa kuwanufaisha matajiri wakubwa na kuwanyima ajira na kipato Wamarekani wengi ni kama ule wa mapatano ya biashara huru nchi za Amerika Kaskazini au North America Free Trade Agreement (Nafta) uliotiwa saini enzi za Rais Bill Clinton wa Democrats.

Kwa mujibu wa wachunguzi wa habari za kibiashara na uchumi, miaka kumi ya Nafta Wamarekani 766,000 wamekosa kazi kwa sababu wamiliki wa viwanda wamefungua viwanda vyao katika nchi za Canada na Mexico badala ya Marekani.

Hillary Clinton anawania urais kupitia tiketi ya chama cha Democrats. Hillary anajulikana kama mtu wa ndani hivyo hata akichaguliwa atalinda masilahi ya wakubwa wa Marekani kama mume wake alivyofanya.

Mikataba mingine ambayo Trump anatishia kuivunja ni pamoja na makubaliano ya jumla kuhusu kodi na biashara yaani General Agreement on Tarrifs and Trade (GATT) wa mwaka 1947 ambao lengo lake ni kupunguza kodi za bidhaa kutoka nje na kukuza biashara duniani.

Ingawa GATT ilikuja kuzaa Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) mwaka 1994 baada ya mazunguko ya Urugway au Urugway Round Agreements, masharti ya GATT bado hufanya kazi chini ya muundo wa WTO.

Mkataba mwingine ambao Trump ametishia kuufutilia mbali ni ule wa Makubaliano ya kibiashara huru kati ya Marekani na mataifa ya Amerika ya Kusini au Central America Free Trade Agreement (CAFTA) uliowekwa saini wakati wa rais Bush mdogo (Bush Jr.) wa Republican mwaka 2005.

Vyama vya wafanyakazi vya Marekani yaani Trade Unions vinapinga mikataba yote hii ambayo inahamisha ajira kutoka Marekani kwenda mataifa ya nje kama vile Amerika ya Kati na Asia.

Hoja yao ni kwamba mikataba hiyo inatoa mwanya kwa wamiliki wa viwanda wa Marekani kuhamishia viwanda vyao huko kufuatia gharama ndogo za uzalishaji katika nhci hizo.

Bidhaa mbalimbali zinazouzwa Marekani hivi sasa hutengenezwa nje ya nchi hiyo na kwa kuwa kuna mikataba hiyo bidhaa hizo hatimaye huingizwa bila ushuru au kwa ushuru mdogo. Matokeo yake uchumi wa Marekani unaathirika.

Kauli za Trump kupandisha kodi za bidhaa kutoka nje na hata kufuta mikataba ya biashara huru kimsingi ni tangazo la vita baina yake na genge linalotawala dunia yaani Globalists.

By Idd Hamis

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad