HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar, inazidi kuwa tete huku siasa za visasi, chuki na uhasama zikionekana kurejea kwa kasi.
Hali hiyo imejitokeza baada ya ofisi za matawi matano ya Chama cha Wananchi (CUF) zilizopo Pemba na moja Unguja kuchomwa moto na watu wasiojulikana.
Matukio ya kuchomwa moto kwa ofisi hizo yamekuja siku mbili baada ya watu wasiojulikana kuchoma moto maskani ya CCM ya Sauti ya Kisonge iliyopo mjini Unguja.
Hata hivyo Jeshi la Polisi visiwani humo limetangaza kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu waliohusika na matukio hayo.
Uchomaji huo ulifanyika usiku wa kuamkia jana saa 8 usiku, ambapo watu hao walichoma moto na kuteketeza nyaraka za chama hicho.
Matawi yaliyochomwa moto ni Kilimahewa mjini Unguja Wilaya ya Magharibi, Mkanyageni, Kiwapwa, Kiuyu Minungwini, Wingwi na Kinowe yote ya Kisiwani Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, amethibitisha kutokeo kwa matukio hayo.
Amesema kutokana na hali hiyo tayari ameagiza askari wake kuanza uchunguzi wa tukio hilo haraka ili waliohusika watiwe nguvuni na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Ni kweli kuna hilo tukio ingawa kwa sasa nipo safari kuelekea Unguja na tayari nimeagiza kuanza kwa uchunguzi wa matukio haya ili wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“…siwezi kusema kama matukio haya yana uhusiano wa masuala ya kisiasa ingawa huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine,” alisema Kamanda Nassir.
Akizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamad (CUF), alilaani tukio hilo huku akiwatuhumu wafuasi wa CCM kuhusika nalo.
Alisema hatua ya CUF kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu imekuwa ikiwaumiza CCM.
“Haya mambo yapo wazi tumeumizwa vya kutosha lakini katika hilo mimi binafsi wala sifichi hapa kuna mkono wa CCM na sisi hatutarudi nyuma tunaendelea na msimamo wa chama,” alisema Hamad.
Kauli ya Maalim Seif
Machi 4, mwaka huu, Akizungumza na wafuasi wake waliomtembelea nyumbani kwake, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema yuko tayari kukamatwa kutokana na msimamo wake wa kutotambua uchaguzi wa marudio.
“Msidhani kuwa mtatupiga shavu la kulia tukawageuzia la kushoto. Kila mara tunaibiwa, tunapigwa, tunafanywa kila kitu. Tukisema kuwa watu wajilinde, inakuwa nongwa.
“…basi tunawaambia kuwa kuitwa polisi, kuwekwa ndani, kufunguliwa mashtaka ya bandia, hata kuteswa, hayo ni mambo yamekuwa yakitutokea tangu 1992 tumeshayazoea,” alisema Maalim Seif.
Alisema udhalilishwaji kama huo haujawahi kukirudisha nyuma chama chake, zaidi ya kukiongezea umashuhuri na ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar, huku akilituhumu Jeshi la Polisi kwa kuwa ‘tawi la CCM’ ambalo litakuwa dhamana wa machafuko yoyote yatakayotokea.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana alirudia msimamo wa chama chake wa kutoshiriki kile alichodai uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, Machi 20, mwaka huu.
Alisema yeye alishashiriki uchaguzi na kushinda na hahusiki kabisa na uchaguzi mwengine. “Ninamwambia Jecha kuwa uchaguzi huo ni wenu peke yenu,” alisema Maalim Seif.