TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amekutana na kufanya Mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoeri Kaguta Museveni, ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Tanga nchini Tanzania hadi nchini Uganda.
Rais Museveni amemtembelea Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Arusha leo jioni mara baada ya kuwasili hapa nchini akitokea nchini Uganda, ambapo hapo kesho atahudhuria Mkutano Mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, utakaofanyika katika Hoteli ya Ngurudoto Jijini Arusha.
Akizungumza baada ya viongozi hao kufanya mazungumzo ya faragha, Rais Magufuli amesema wamekubaliana kutekeleza mradi huo wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Tanga hadi Uganda, kwa manufaa ya nchi zote mbili na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Amesema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,120 na kwamba mradi huo utazalisha ajira za watu zaidi ya 15,000.
Rais Magufuli ameongeza kuwa pamoja na kujengwa kwa bomba la mafuta, pia wamezungumzia kuongeza biashara ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda na kuzalisha ajira zaidi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Aidha, Rais Magufuli amesema katika Mkutano huu nchi wanachama watajadili maombi ya nchi ya Sudan Kusini kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.