Hotuba Ya Kwanza Ya Ole Sendeka Kama Msemaji Wa CCM

Machi 15, 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli akiwaapisha Wakuu wapya wa mikoa, aliagiza pamoja na mambo mengine, viongozi katika ngazi mbalimbali kuhakikisha wanasimamia nguvu kazi ya vijana katika maeneo yao ili waache kukaa kijiweni.

Agizo hilo lililenga utekelezaji wa vitendo wa matumizi bora ya rasilimali watu nchini wakiwemo vijana ambao ni nguvu kazi muhimu kwa taifa, kujengewa mazingira mazuri yatakayowawezesha kujiajiri katika shughuli za uzalishaji mali.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinampongeza kwa dhati Rais Magufuli kwa agizo lake hilo lenye lengo muhimu la kuwafanya watanzania kwa pamoja kuwajibika.

CCM inampongeza Rais Magufuli kwani kwa mara nyingine tena amedhihirisha kuwa wapiga kura walio wengi walifanya uamuzi sahihi kwa kumchagua yeye kuwa Rais wa Serikali
ya awamu ya Tano katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

CCM kama chama anachotoka Rais Magufuli na ambacho ndicho Ilani yake inatekelezwa na serikali kwa kupindi cha 2015/2020, ina kila sababu ya kumpongeza kwa kuanza
vizuri katika uongozi wake wa miaka mitano na tunaamini kuwa katika kipindi hicho, “Tanzania Tunayoitaka” itafika mbali kimaendeleo kwenye kila ngazi.

Historia ipo wazi kuwa wakati Tanzania inapata uhuru wake mwaka 1961, Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliongoza taifa letu na kauli mbiu ya UHURU NA KAZI baadae ikabadilika kuwa Uhuru ni Kazi na sasa awamu ya Tano inaendesha shughuli zake kwa kauli mbiu ya “HapaKaziTu” ambayo kila mmoja ni shahidi kuwa hivi sasa kazi inatekelezwa kwa kasi kubwa.

Utekelezaji wa kauli mbiu ya HapaKaziTu umejidhihirisha katika kipindi kifupi cha uongozi wa Serikali hii yak awamu ya tano katika kudhibiti rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya madaraka na na ukwepaji kodi, mambo ambayo matokeo yake yameshaanza kuonekana.

Matokeo hayo ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya kodi ya serikali, ambayo yameiongezea serikali uwezo wa kuwahudumia wananchi kujikwamua na umaskini kwa
ustawi wa jamii kwa ujumla.

Aidha CCM kinamuunga mkono Rais Magufuli pia kwa hatua anazozichukua yeye na serikali yake katika kurudisha nidhamu na uwajibikani katika utumishi wa umma.

Kumbukumbu zinaonyesha mpaka sasa watumishi wa umma waliochukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma mbalimbali kwenye utumishi wao, na wengine wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria, wamefanyiwa hivyo kwa kufuata sheria na kuzingatia misingi ya utawala bora.

Hata hivyo wapo watu wachache wameamua kupotosha nia njema ya Mheshimiwa Rais na serikali yake kwa kuonesha kuwa haya yanayofanyika ni udikteta na uonevu.

Naomba ifahamike kuwa CCM iliiagiza serikali yake kwenye ilani yake ya uchaguzi ya 2015/2020 kuhakikisha inarudisha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma kwa hiyo kinachofanywa na Rais Magufuli na serikali yake ni utekelezaji ilani ya CCM na ndiyo mahitaji na matakwa ya watanzania walio wengi.

Watanzania walio wengi wanataka kuuona utumishi wa umma wenye nidhamu na uwajibikaji hivyo tunawaomba watanzania kuwapuuza wale wote wanaotafsiri hatua hizi kuwa ni udikteta na uvunjifu wa sheria, kwani kwa matendo yao na maneno yao wanashabikia uzembe na kutowajibika kazini jambo ambalo CCM haikubaliani nalo.

CCM inawasihi wanachama wake, wapenzi, wakereketwa, mashabiki na watanzania wote kwa ujumla kuwa mstari wa mbele kumuunga mkono kwa vitendo Rais Magufuli kwa dhamira njema aliyonayo kwa taifa letu, ili hatimaye Tanzania yenye maendeleo ifanikiwe.
………………………………………………………………………

Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,

20/03/2016

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad