Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama amewataka wananchi kuvuta subira kuhusu uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa sababu mamlaka za juu zitamteua wakati mwafaka ukifika.
“Niliteua kaimu mkurugenzi wa NSSF, uteuzi ukatenguliwa kwa sababu baadhi ya taratibu zilikuwa hazijakamilika, the business is over (biashara imekwisha), tusubiri mamlaka za juu zitafanya uteuzi, mna haraka ya nini?” alihoji Mhagama.
Alipoulizwa nani anayesimamia uendeshaji wa shirika hilo kwa sasa, Mhagama alisema: “Jamani, nimeshasema tusubiri mamlaka za juu, sina cha kuongeza.”
Waziri Mhagama alimteua Dk Carina Wangwe kukaimu nafasi hiyo lakini uteuzi huo, ulidumu kwa saa tano na kutenguliwa.
Nafasi hiyo ipo wazi tangu Februari 15, baada ya Rais John Magufuli kumteua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau kuwa balozi.
Ripoti NSSF yatia shaka
Awali, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilisema ripoti ya utendaji ya NSSF iliyofikishwa mbele yake haina viwango kama ambavyo mfuko huo unavyoonekana mbele ya jamii.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Omar Mchengerwa alisema taarifa zilizomo kwenye ripoti hiyo hazionyeshi miradi inayoendelezwa na mfuko huo.
“Tumeipokea na kuijadili kwa sababu ya kuheshimu kazi zinazofanywa na mfuko na uwapo wa Waziri Mhagama, vinginevyo tungewatoa nje mkaifanyie marekebisho,” alisema.
Hata hiyo, Mchengerwa aliagiza watendaji wa shirika hilo kupeleka ripoti yenye taarifa kamili ifikapo Machi 31. “Tunataka tukiisoma taarifa tunaijua vizuri NSSF, miradi yake yote na thamani yake, nyie mnatuletea taarifa fupi ambayo haina majibu ya maswali tunayoyataka,” alisema.
Katika taarifa hiyo, mfuko huo unalalamikia wanachama wengi kujitoa mara wanapomaliza mikataba na waajiri wao na kuhitaji mafao kabla ya umri wa kustaafu.
NSSF inasema kumekuwa na ongezeko kubwa la mfuko kulipa mafao wanachama wa aina hiyo na kwamba, miaka michache ijayo kutakuwa na wastaafu wengi ambao hawana mafao ya uzeeni hivyo kuwapo wazee wengi wasio na kipato.
Akifafanua hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori alisema kuna haja ya Serikali kurudisha sheria ya kuzuia wanachama kujitoa kabla ya kufikisha umri wa kustaafu.
Magori alisema wazee wengi ambao hawana mafao ya uzeeni wanakufa haraka, kuliko wanaolipwa mafao kila mwezi.
“Kuna takwimu zinaonyesha ukubwa wa tatizo hilo, Serikali inatakiwa kurudisha sheria na kuzuia wanachama kujitoa kwenye mifuko kwani wao wenyewe ndiyo watakaoumia uzeeni,” alisema.
Naye Waziri Mhagama aliwaagiza watendaji wa mfuko huo kutayarisha ripoti ambayo itakusanya miradi yote inayoendelezwa.