Machangudoa Wanne Kati ya Kumi Wanaojiuza Wanamaambukizi ya Virusi vya Ukimwi.....

Utafiti uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na upimaji wa virusi vya Ukimwi la MATUMAINI, unaonyesha kuwa kati ya wanawake kumi wanaofanya biashara ya ngono wanaopima wanne kati yao wanakutwa na virusi vya Ukimwi.

Akizungumza na East Africa Radio Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bw. Onesmo Mwihava amesema wamekuwa wakifanya zoezi la upimaji katika maeneo ya majumba ya starehe, baa na katika baadhi ya madanguro yasiyo rasmi na kuwa licha ya kuwepo kwa jitihada za serikali katika kutokomeza biashara ya ngono lakini wengi wa wanaojiuza wanakutwa wameathirika ama kuwa na magonjwa ya zinaa.

Aidha, Bw. Mwihava amesema kuwa watu wengi wamekuwa wakijihadhari na suala la kupata mimba na kuacha kuchukua tahadhari kuwa katika kupata maambukizi pamoja na magonjwa ya zinaa ambapo katika utafiti wao, kati ya watu kumi waliojitokeza kupima kati yao sita huwa na magonjwa ya zinaa.

Ameongeza kuwa mojawapo ya waathirika wakubwa wa ugonjwa wa ukimwi pamoja na magonjwa ya zinaa ni vijana kutokana na kutochukua tahadhari kwa kufanya ngono zembe na kuwa hali hiyo mara nyingi hutokana na kiwango cha fedha alizotoa kwaajili ya huduma hiyo.

Mwihava amezitaka taasisi na serikali kulivalia njuga suala la kutokomeza biashara ya ngono pamoja na kutoa elimu kwa vijana na wanaojihusisha na vitendo hivyo haswa baada ya kukamatwa kwakuwa kwa sasa wanawake hao wengi wameanzisha mbinu mpya kwa kukaa katika baa na majumba ya starehe na kutoka na wateja.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad