Magufuli: Afrika Mashariki Haipaswi Kuwa Maskini

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Rais John Magufuli jana alizindua barabara ya Afrika Mashariki akibainisha kuwa wananchi wa nchi za jumuiya hiyo hawapaswi kuwa maskini kwa kuwa mradi huo na mingine itakayotekelezwa itasaidia kuinua hali ya maisha.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa barabara hiyo ya Arusha - Holili/Taveta - Voi yenye urefu wa kilomita 234.3, Rais Magufuli alisema watu wa Afrika Mashariki hawana shida na vyama, bali wanataka maendeleo.

Katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Rais Yoweri Museveni (Uganda), Rais Uhuru Kenyatta (Kenya) na wawakilishi wa marais wa Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, Dk Magufuli alisema watu wa Afrika Mashariki wanataka ajira hivyo mambo ya kuwafanya wachache kuwa na mali nyingi na wengi kuwa maskini lazima yaishe.

“Sisi kama marais wa Afrika ya Mashariki tumejipanga kuhakikisha tunabadilisha maisha ya wananchi,” alisema Rais huyo aliyekabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo juzi.

Alisema anataka kuona Afrika ya Mashariki yenye viwanda ambavyo vitasaidia kupatikana ajira kwa vijana na kukuza uchumi.

Alisema ni lazima nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zinazounda jumuiya hiyo ziondokane na tabia ya kuombaomba wakati zina rasilimali za kutosha.

Alisema asilimia 63 ya vijana katika nchi za Afrika ya Mashariki, hawana ajira ndiyo sababu juzi wakuu wa nchi hizo wamefikia makubaliano ya kuhakikisha wanafufua na kujenga viwanda katika nchi zao.

“Hakuna sababu ya pamba inayolimwa Jinja (Uganda), iende Ulaya kutengeneza nguo na ajira kwa vijana wao na nguo ambazo wanavaa Wazungu wakizichoka wanazirejesha kwetu kama mitumba,” alisema.

Alisema lengo la sasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuona pamba inalimwa na inatengeza nguo ambazo zinavaliwa hapa na nyingine kuuzwa nje.

Rais Magufuli alisema wanataka kuona madini ya chuma ambayo yanapatikana Afrika ya Mashariki yanatumika kutengeneza magari na kuuza nchi za Ulaya.

“Tanzania tuna ng’ombe zaidi ya milioni 22, lakini tunauza ngozi nje ambayo haijaongezewa thamani na wao wanatengeneza viatu bora wanavaa, sisi huku wanatuletea viatu vya magome ya miti ambavyo havidumu, tunataka kuondoka katika hali hii,” alisema.

Aliwataka wananchi kuwaamini na kuwasaidia viongozi wao akisema wanaweza kuleta mabadiliko katika jumuiya hiyo ambayo ina watu zaidi ya milioni 160 baada ya Sudan Kusini kujiunga.

Alisema kimsingi nchi za Afrika ya Mashariki si maskini kwa kuwa zimejaaliwa rasilimali nyingi ambazo zingeweza kutumika vyema kuwasaidia wananchi.

“Tumeambiwa Sudan Kusini kuna madini ya aina 22, hapa Tanzania tuna madini mengi, yakiwamo tanzanite lakini ukienda Mererani maisha wanayoishi watu wa eneo hilo huwezi kuamini,” alisema.

Rais Museveni alisema nchi za Afrika si maskini, bali kuna tatizo la kukosa maendeleo.

Alisema ili nchi za Afrika Mashariki ziendelee, zinahitaji vitu vitatu, kilimo cha kisasa, viwanda na matumizi ya teknolojia ya kompyuta.

Rais Kenyatta alisema kuwa nyuma kwa nchi za Afrika ya Mashariki kumetokana na Serikali husika kuwa nyuma katika kuwasaidia wananchi kufanya biashara na hivyo kupata usumbufu kutokana na kujali mipaka ya kila nchi.

“Haitawezekana kupata maendeleo tukiendelea na hii mipaka iliyowekwa na Wazungu, mipaka ya nchi ilichorwa na Mjerumani ambaye hakuwahi hata kufika katika nchi hizi,” alisema akimaanisha kuwa biashara inatakiwa kuvuka mipaka. Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini, James Wani Igga aliwataka wakazi wa Afrika ya Mashariki kutoiona nchi yake kama mzigo kwao baada ya kuwa mwanachama juzi akisema ina ardhi kubwa yenye rutuba, madini na hivyo ni moja ya maeneo ambayo wananchi wa nchi hizo wanaweza kwenda kuwekeza.

Barabara yenyewe

Akizungumzia barabara hiyo, alisema kwa upande wa Tanzania, Sh209.3 bilioni zitatumika katika ujenzi wa barabara ya kilomita 14.1 ya njia nne ya Arusha - Tengeru na fedha nyingine zitatumika kwa barabara ya nje ya mji wa Arusha yenye urefu wa kilomita 42.3.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh109 bilioni zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (Jaica) na Sh19.4 bilioni zimetolewa na Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.  

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad