Alikuwa anatambulika kutokana na uigizaji wake tangu akiwa binti wa miaka mitano na umahiri wa kuvaa vyema uhalisia wa nafasi anazopewa kuigiza, jambo lililomtengenezea mashabiki wengi.
Umaarufu hauna tofauti na mvua za masika ambazo zinaweza kuleta neema au maafa kwa mafuriko. Wanaomfahamu Lulu tangu akiigiza kama mtoto katika tamthilia za Kundi la Kaole Sanaa Group hawahitaji kusimuliwa. Wengine wanasema majina yanaponza kwa maana ukiwa maarufu jambo lako dogo litashupaliwa lionekane kubwa. Kuna wakati Lulu alikuwa habari ya mujini kwa Kiingereza tungesema She was on top of her game.
Uigizaji na utangazaji wa Kipindi cha Watoto Wetu kilichokuwa kikirushwa na kituo cha ITV mwanzoni mwa miaka ya 2000 vilimjengea umaarufu.
Awali alipamba vichwa vya habari kwa kufanya vema katika maigizo na filamu, baadaye alipamba vichwa hivyo kwa habari nyingine ambazo hazina uhusiano kabisa na filamu na sasa amerejea akiwa na habari kubwa kuliko zote ambazo waigizaji wengi wameshindwa kufikia lengo hilo.
Pengine mwenyewe aligundua nini kilikuwa kinatokea katika maisha yake ndiyo maana akaamua kuachia filamu aliyoibatiza jina la “Foolish Age”. Huyu si mwingine bali ni Elizabeth Michael ambaye anafahamika zaidi Afrika Mashariki na Kati kwa jina moja la Lulu.
Jina la Lulu alipewa na Chiki Mchome ambaye mbali na kumtaka alitumie katika filamu yake, alimsihi alitumie kibiashara kwani litamfungulia milango ya neema siku za usoni.
Maandalizi, ujasiri, kujitambua , kujituma kumemfanya aibuke kidedea katika tuzo kubwa za filamu barani Afrika za Africa Magic Viewers’ Choice (AMVCA), kupitia filamu yake ya “Mapenzi ya Mungu”. Filamu ambayo kwa madai ya mwigizaji huyo kisa na hadithi yake inaendana na maisha yake.
Kwa nini alilia?
Maneno machache yalisikika wakati akitoa neno la shukrani baada ya kupokea tuzo yake, mengi yalimezwa na kilio alichokitoa.
Sikulia kwa uchungu, nililia kwa furaha na huzuni pamoja, kama nilivyohuzunika wakati wa kuigiza filamu ya “Mapenzi ya Mungu” ambayo maarufu Mapenzi ndivyo nilivyolia wakati nachukua tuzo.
Kushinda tuzo kubwa kama ile siyo kitu kidogo, nilikuwa nina kila sababu ya kulia ukizingatia nimekuwa msanii wa kwanza wa kike kuipata, ahsanteni Watanzania na mashabiki wangu kwa kuniunga mkono.
2016
Mwaka ambao Lulu amejitofautisha na waigizaji wengine wa kike kutokana na kunyakua tuzo ya kubwa Afrika katika kipengele cha filamu bora Afrika Mashariki kupitia filamu yake ya “Mapenzi ya Mungu”. Ameibuka kuwa mwigizaji wa kwanza kutoka nchini Tanzania kushinda tuzo hiyo na kuwapiku magwiji wa filamu nchini.
2015
Mwaka huu ndiyo ulikuwa msingi wa mafanikio ambayo Lulu anayofurahia leo. Huu ndiyo mwaka aliotoa filamu yake ya Mapenzi ya Mungu ambayo ndiyo ilimtoa kimasomaso katika tuzo hizo. Hii ilikuwa ni kazi yake ya tatu baada ya kutoa “Foolish Age” zote zikiwa chini ya Kampuni ya Usambazai Filamu ya Proin Promotion.
Mwigizaji huyo alidhamiria kusimama na kuonyesha kuwa amejifunza kitu kutokana na misukosuko aliyopitia, baada ya kujiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni Jijini Dar es Salaam.
2014
Lulu ana cha kujivunia katika mwaka huu pia kutokana na kuibuka kidedea katika Tuzo za Watu, ambapo alishinda kipengele cha msanii bora wa kike anayependwa. Kutokana na kupata tuzo hiyo alizidi kujiongezea umaarufu na kuwa gumzo huku akifanya mambo yake kimya kimya na kujiondoa kwenye makundi ya wadada wa mjini.
Aliweza kujitofautisha na wasanii wengine kwa kuishi maisha ya kistaa, mpangilio wa mavazi, nywele, viatu na mikoba hivyo vyote vilitosha kumfanya Lulu avute mashabiki wengi kwenye ukurasa wake wa Instagram.
2012/13
Aliiibuka kinara katika kinyang’anyiro cha mwigizaji bora wa kike katika Tamasha la Zanzibar International Festival (ZIFF), kutokana na umahiri alioonyesha wakati akiigiza filamu ya “Women of Principles”.
Kama nyota imeng’aa, mwaka huo huo alifanya uzinduzi wa kishindo wa ujio wake mpya baada ya kutoka katika mikasa ya kusota rumande, alifanya uzinduzi wa filamu yake mwenyewe iitwayo “Foolish Age” na “Family Curse”.
Alianza lini kuigiza?
Elizabeth Michael lulu akiwa na miaka mitano.Muigizaji Mahsein Awadh, “Dk. Cheni”ndiye aliyemuibua kupitia bonanza la kuibua vipaji lililoandaliwa na nyota huyo aliyekuwa akiigiza katika kundi la Kaole.
By Kalunde Jamal, Mwananchi
MAKALA:Kupanda, Kushuka na Kuibuka Tena Kwa Mwigizaji Mrembo Lulu Michael.....
0
March 15, 2016
Tags