Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija na kamati yake ya utendaji kuvuliwa madaraka kutokana na msuguano baina yao, wajumbe wa mkutano Mkuu wa chama hicho wamemtaka Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe kuingilia kati mgogoro huo.
Mwambigija na viongozi wengine akiwamo katibu wa chama wilaya, katibu mwenezi na wajumbe wengine wa kamati ya utendaji wilaya, walivuliwa nyadhifa zao hivi karibuni baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika usiku chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa Zanzibar, Issa Said Mohamed.
Akizungumzia kuvuliwa uongozi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Hezron Mwaisengela ambaye pia ni Katibu Kata ya Mwakibete, alisema hawakubaliani na uamuzi wa kuivua madaraka kamati ya utendaji kwa kuwa hawakushirikishwa. “Kilichofanyika hakikubaliki na ni uvunjaji wa Katiba ya chama na tukiendelea kulea upuuzi huu, tutavurugana kabisa.
“Viongozi hao walichaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu ambao ni sisi na hata kuondolewa kwa namna yoyote ile ni lazima uitishwe mkutano mkuu kinyume na hapo sisi tunaendelea kuwatambua viongozi hawa,” alisema Mwaisengela.
Mjumbe mwingine, Frank Mwankina ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Kata ya Nzovwe, alisema wapo kwa ajili ya kulinda masilahi ya chama na siyo vinginevyo.
“Kama kuna ukweli wowote kuhusiana na tuhuma hizo walipaswa kujadiliwa kwenye vikao rasmi,” alisema Mwankina.
Alisema Mbowe aliyefika hivi karibuni mkoani humo kusikiliza mgogoro huo, alipokea malalamiko ya kila upande, lakini hawakupaswa kuwavua madaraka ambayo waliyapata kwa kuchaguliwa.
Kauli za wajumbe hao zinatolewa wakati hali ya Chadema jijini hapa ikizidi kuwa tete kutokana na madiwani kuhasimiana.
Mpasuko Chadema..Wamtaka Freeman Mbowe Akanusuru Jahazi Mbeya Mjini...
0
March 01, 2016
Tags