Mtoto wa Miaka Sita Auawa Kwa Kupigwa na Mpini wa Jembe Kichwani...

Polisi mkoani Mwanza inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji yakiwamo ya mtoto wa miaka sita kwa kupigwa na mpini wa jembe kichwani.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Justus Kamugisha alisema kuwa mkazi wa Gulumungu wilayani Misungwi anashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mtoto huyo, Zawadi Shija (6).

Kamugisha alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kama njia ya kumkomoa bibi wa mtoto huyo, Samaka Mashala ambaye wanagombea mpaka wa shamba.

Alisema tukio hilo lililozua simanzi miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho lilitokea Machi 9.

Alisema kabla ya kuuawa, Zawadi alitumwa dukani na dada zake, lakini alichelewa kurejea nyumbani hali iliyosababisha aingiwe hofu ya kuadhibiwa na kuamua kujibanza nyuma ya nyumba ya jirani yao.

“Yule jirani alipomuona mtoto yule amejibanza nyuma ya nyumba, alihamaki na kuanza kumshambulia kwa mpini wa jembe na kumsababishia majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake wakati anapatiwa matibabu Kituo cha Afya Misasi,” alisema.

 Wivu wa mapenzi waua

Katika tukio jingine; Kamanda Kamugisha alisema wanamshikilia mkazi wa Kijiji cha Bukokwa wilayani Segerema kwa tuhuma za kumshambulia hadi kufa, Boniface Mwitwa baada ya kumtuhumu kuwa na uhusiano wa mapenzi na mkewe.

Alisema Machi 7 mwaka huu, mtuhumiwa huyo alimkuta Mwitwa akizungumza na mkewe, Tabu Misalaba na kumshambulia hadi kufa.

Kwa mujibu wa Kamugisha, Mwitwa aliwahi kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanamke huyo, walifanikiwa kupata mtoto hali iliyokuwa ikimpa wivu mumewe kila akiwakuta wawili hao wakizungumza kuhusu mtoto wao huyo.

Kamanda Kamugisha aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, hivyo kufuata taratibu kwa mwenye malalamiko kuyafikisha kwenye vyombo vya sheria ili kupata haki yake.

Migogoro ya mashamba imekuwa ikisababisha mauaji hasa kwa vikongwe kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, hali inayosababisha kanda hiyo kukithiri kwa mauaji hayo.

Pia, wivu wa mapenzi ni chanzo kingine cha mauaji ambayo kwa mikoa ya kanda hiyo hutokea karibu kila wiki na kusababisha mauaji ya watu na wengine kujeruhiwa.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad