Mzee Yusuf, Watulize Wake zako! Wanachofanya Mitandaoni ni Aibu Kwako

KWAKO Big Boss wa Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuf, habari za siku? Uko poa? Pole na majukumu ya kila siku.

Wajionaje na hali? Familia yako kwa ujumla haijambo? Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima wa afya. Namshukuru Mungu. Napata haki yangu kupitia taaluma yangu na maisha yanazidi kuyoyoma.

Madhumuni ya kukuandikia barua hii ni kutaka kukueleza kwamba sikufurahishwa sana na mgogoro ulioendeshwa na wake zako ambao kimsingi niliamini ulikuwa unaweza kuepukika kabla ya kuwafaidisha watu.

Wiki iliyopita haikuwa nzuri sana kwako. Kwa kuwa Watanzania wanakuheshimu, wanakuamini naamini hawakufurahishwa na malumbano yaliyoibuliwa na wake zako. Naamini hata wewe hayakukufurahisha. Ndoa yako imejadiliwa sana mitandaoni.

Mmewapa sana nafasi watu kuzungumza vitu ambavyo havikuwa na sababu ya kuzungumzwa.
Kutukanana, kushutumiana mambo mazitomazito halikuwa jambo jema. Ilileta picha mbaya kwa mashabiki wako na wale wa Jahazi. Kama baba, ulipaswa kulidhibiti kabla halijatoka nje.
Nasema hivyo kwa sababu vitu ambavyo walianza kuvizungumza vilikuwa ni vya kujidhalilisha wao wenyewe na wewe pia.

Kwa kuwa wote ni wake zako, ulikuwa na nafasi ya kuwakanya wasitoe siri za ndani. Kuwaambia wote wasizungumze na vyombo vya habari maana kufanya hivyo kulilifanya sakata hilo kuzidi kuwa kubwa.

Badala yake ugomvi ulikuwa mkubwa. Watangazaji nao wakadandia sakata hilo. Kila mmoja akawa na upande wake, mwisho wa siku ilikuwa ni fedheha kwa familia yako.
Sakata hilo limewafanya hata ambao hawakuwa na wazo la kujadili maisha yenu binafsi, kuanza kufanya hivyo. Nakushauri kama bado hujaamua, amua sasa. Kaa nao chini na kubaini kiini cha ugomvi. Kujua nani alianza na nini ufanye ili uweze kumaliza tofauti.
Wanawake ni mama zetu, lakini tunafahamu mara nyingi huwa ni rahisi kukuza ugomvi mdogo na kuufanya uwe mkubwa. Pengine chanzo kilikuwa ni kidogo, waeleze ukweli kwamba hawapaswi kuyatoa nje mambo yao.

Waeleze kwamba madhara ya hivyo ni kujidhalilisha na kuwafanya waonekane hawajafundishwa na wazazi wao. Waeleze kwamba wewe ni nani, una heshima gani katika jamii, hivyo waishi kulingana na heshima yako. Waache mambo yale ya ‘kiswahili’.

Ikiwa unaona unazungumza kama mume na bado mmoja wao au wote wanakuwa hawakuelewi, ni vyema kuchukua hatua kali zaidi. Heshima yako umeijenga kwa muda mrefu, ni vyema kushirikisha hata wazazi kusaidia kutatua mgogoro huo.

Simama kama mwanaume. Kuwa mkali pale inapobidi kufanya hivyo maana wakati mwingine wapo baadhi ya wanawake wanaojaribu kutikisa kiberiti ili waone ndani kina nini. Ukiwa mkali, utamuona amenywea.

Nakuamini maana ni muda mrefu uliweza kudhibiti mikwaruzano ya kifamilia kutoka nje. Naamini katika hili imepenya bahati mbaya. Unajua wapi imepenyea, basi jitahidi kudhibiti isitokee tena siku za usoni.

Ni matumaini yangu utasimama kama mwanaume na mgogoro huo utaisha na hata siku nyingine hatutasikia mambo binafsi yanatoka katika vyombo vya habari.
Mimi nduguyo;
Erick Evarist
Global Publishers

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hv wewe kila siku unashauri watu na kuwaandikia barua...we nani anakukosoa na kukuandikia barua...hovyooo unaboa mnoo we na bosi wako wa global wambea wambea tu kazi kuyaona ya watu yenu mmeyafukia

    ReplyDelete
  2. ndio shida ya uke wenza yani nivita hadi mwisho wa dunia raha kuishi na mmoja tu

    ReplyDelete
  3. Sasa kama mmeyaleta wenyewe uwanjani ndo yasiandikwe na ww chizi nini?Kukaa uchi ukae uchi mwenyewe halafu unalalamika kwa nini watu wanakutazama uchi wako alaaaahhhhh!!!!!!Mambo ya ndani ya ndoa mnayapeleka instagram ili iweje.......nyie wanawake mwalimu wenu kipofu na alowaroga kashakufa abadani. Acha ashauri na kukosoa pale panapobidi na penye ukweli kwani tunaamini asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.....global publishers ni sehemu ya ulimwengu acha afanye kazi yake.....

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad