Nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) inaonekana kuwa moto baada ya mfuko huo kumaliza siku ya 22 bila ya kuwa na mbadala wa Dk Ramadhan Dau au kaimu wake.
Jaribio la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama kuziba nafasi hiyo kwa muda lilidumu kwa saa tano tu baada ya kulazimika kutengua uteuzi wa Carina Wangwe Alhamisi iliyopita.
Waziri Mhagama alilazimika kutengua uteuzi huo kwa maelezo kuwa taratibu zilikosewa huku Balozi Ombeni Sefue akieleza kuwa mkurugenzi huyo wa Tehama wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA) alitakiwa kuwa msimamizi tu na si kaimu mkurugenzi.
Jana, juhudi za gazeti hili kutaka kujua maendeleo ya uteuzi wa mtu mpya wa kushika nafasi hiyo ziligonga mwamba.
Balozi Sefue, ambaye hadi jana alasiri alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, hakutaka kuzungumzia suala hilo akimuelekeza mwandishi kumtafuta Waziri Mhagama.
Lakini Waziri Mhagama hakuweza kupatikana licha ya kutafutwa mara kadhaa. Juhudi za kumpata kwa simu zilishindikana kwa kuwa hakuwa akipokea na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu.
Pamoja na kuteuliwa kuwa balozi ambaye atapangiwa kituo baadaye, Dk Dau aliondoka NSSF kwa njia ambayo imewaacha wengi wakiwa midomo wazi.
Akiongoza kikao cha viongozi wa mikoa wa NSSF jijini Dar es Salaam, Dk Dau aliletewa taarifa kuwa alikuwa akihitajiwa na mtu muhimu na hivyo kulazimika kumuachia kikao mmoja wa wakurugenzi wake, kwa mujibu wa habari ambazo Mwananchi imezipata.
Dk Dau hakurejea tena kikaoni na baadaye habari zikitangazwa kutoka Ikulu kuwa ameteuliwa kuwa balozi pamoja na Asha Rose Migiro na Mathias Chikawe.
Habari zinasema kuwa wiki iliyofuata, Dk Dau alianza kuonekana ofisini kabla ya kutaarifiwa kuwa uteuzi wake ulianza mara moja hivyo aachane na kazi za NSSF.
Kutokana na mazingira ya kuondoka kwake, hakuna mtu anayekaimu nafasi yake kati ya wakurugenzi nane walio chini ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF.
Habari zinasema kuwa mazingira hayo yamesababisha kuzorota kwa shughuli za shirika hilo kubwa kuliko yote yanayojihusisha na hifadhi ya jamii.
Miongoni mwa mambo hayo ni ufunguzi wa daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam ambalo lilitakiwa lianze rasmi kutumika Machi Mosi, ununuzi wa magari ya ofisi za mikoa, mkutano wa wanachama wa mwaka pamoja na wiki ya NSSF ambayo hujumuisha mambo mbalimbali, kama shughuli za kijamii, maonyesho ya huduma za NSSF na michezo.
Wiki iliyopita Balozi Sefue alisema maswali kuhusu uteuzi wa kaimu yaelekezwe kwa Mhagama, ambaye alieleza wakati huo kuwa utaratibu wa kumpata kaimu ulikuwa unaendelea.
Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya mwaka 2011, shirika hilo lilikuwa na wanachama 501, 218, kati yao wafanyakazi waliosajiliwa waliongezeka kutoka 17,666 hadi 18,779, sawa na ongezeko la asilimia 6, huku michango ikiongezeka kutoka Sh300.08 bilioni hadi Sh356.5 bilioni kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.8.
Kwa mujibu wa muundo wa uongozi wa NSSF, Mkurugenzi Mkuu ndiye kiongozi mkuu wa shirika akiwa na wakurugenzi nane chini yake.
Wakurugenzi hao wanahusika na uendeshaji (DO); utawala na rasilimali watu (DHRA); mipango, uwekezaji na miradi (DPIP); fedha (DF); teknohama (DIT); ukaguzi wa ndani (DIA); uthibiti na usalama wa mali (DARM) na huduma za kisheria (DLS).
Dk Dau, ambaye amebobea katika taaluma ya masoko, ameliongoza shirika hilo kwa miaka 15, tangu mwaka 2001 alipoteuliwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.