Katika kile kinachoonekana kuwa ni kumchokoza waziwazi Rais John Magufuli, Ofisa wa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni ametoa agizo la kuwataka wakuu wote wa shule za sekondari kwenye manispaa yake kukata Sh. 1,500 kwa kila mwanafunzi kutoka katika fedha wanazopokea kwa ajili ya uendeshaji wa shule zao na kisha kuzipeleka kwenye manispaa hiyo.
Katika barua ya Februari 4, 2016 iliyosambazwa kwenda kwa walimu wakuu wa shule za sekondari za Kinondoni na Ofisa wa Elimu wa Manispaa hiyo aitwaye Rogers Shemwelekwa, inaelezwa kuwa fedha hizo zinapaswa kutolewa na kila mkuu wa shule ili kugharimia michuano ya sekondari, inayoandaliwa chini ya mwavuli wa Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA). Amri iliwataka wakuu wote wa shule za sekondari Kinondoni zikiwamo pia zinazomilikiwa na taasisi binafsi kuwasilisha michango hiyo ifikapo Februari 28 kupitia akaunti namba 0150259059100, katika benki ya CRDB kwa jina la KMC Miscellaneous deposit Account na stakabadhi zote zipelekwe kwa Ofisa Elimu wa Sekondari. Michezo hiyo ya UMESSETA inatarajiwa kuanza Mei.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa agizo hilo linakwenda kinyume cha waraka wa serikali kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku zinazotolewa kila mwezi kwa ajili ya kufanikisha utoaji wa elimu bure iliyoahidiwa na Rais Magufuli wakati wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Kwa mujibu wa waraka wa kufanikisha elimu bure, fedha zilizoguswa kupitia agizo la Ofisa Elimu wa Kinondoni zipo katika fungu la pili ambalo lililotengewa asilimia 30 ya fedha zote za ruzuku kwa lengo la kuziwezesha shule siyo kugharimia michezo peke yake bali pia ukaguzi na vifaa vya kujifunzia.
Tangu Januari mwaka huu, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imekuwa ikisambaza fedha za kufanikisha utoaji wa elimu bure kwa kila shule kuanzia msingi hadi kidato cha nne, lengo likiwa ni kuwaondolea wananachi kero ya kukabiliana na rundo la michango kwa visingizio mbalimbali vikiwamo vya michezo, madawati, ulinzi, uji, nembo ya shule, majengo karatasi, maandalizi ya mitihani, umeme, maji na masomo ya ziada marudu kama ‘tuition’. Katika mgawo wa kwanza uliotolewa Januari, serikali iligawa Sh. bilioni 18.77 kwa ajili ya kugharimia elimu bure nchini kote huku Rais Magufuli akionya kuwa ole wake atakayekiuka maelekezo na kubadilisha matumizi ya fedha hizo.
Wakizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, baadhi ya walimu wakuu wa shule za sekondari katika manispaa ya Kinondoni wamelalamikia hatua hiyo ya kutakiwa walipe Sh. 1,500 kwa kila mwanafunzi kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha agizo la Rais kuhusiana na utoaji wa elimu bure.
Walimu hao, kwa nyakati tofauti walisema kuwa wao hupokea fedha moja kwa moja kutoka Hazina zikiwa zimewekewa maelekezo, lakini wanashangaa kuona Shemwelekwa anawapa maagizo yanayokiuka maelekezo ya Hazina kwa kuwaagiza kwamba wakishazipata, wahakikishe wanazipeleka Manispaa kwa ajili ya kugharimia michezo, tena kwa kiwango mahsusi cha Sh. 1,500 kwa kila mwanafunzi.
Baadhi ya walimu wakuu walisema ingawa idadi ya wanafunzi kwa kila shule ndiyo kigezo cha kupokea mgawo mkubwa au kidogo, lakini kwa wastani, asilimia 30 ya ruzuku wanayopewa na serikali na ambayo hujumuisha pia shughuli za michezo na ununuaji wa vifaa vya kujifunzia huwa haifiki Sh. 600,000 kwa mwezi.
Mmoja wa walimu alitolea mfano wa shule yenye wanafunzi 1,000, akisema kwamba endapo wakitii agizo la Ofisa Elimu Shemwelekwa, maana yake shule ya aina hiyo inapaswa kulipa Sh. milioni 1.5 kwa ajili ya michezo na kiasi chote kinapaswa kulipwa kwa wakati mmoja.
Mwalimu mwingine aliiambia Nipashe kuwa kwa ujumla, shule moja hupata wastani wa Sh. 1,700,000 kila mwezi kugharimia elimu bure na hivyo, ikiwa fedha hizo zitatolewa kwa wakati mmoja, maana yake uendeshaji wa shule zao utasimama kwa mwezi mmoja kwa sababu kiasi cha fedha kitakachobaki kitakuwa ni kidogo na kamwe hakiwezi kufanikisha utoaji wa elimu pasi na kuhitaji michango kutoka kwa wazazi.
OFISA ELIMU AKIRI, ARUSHA MPIRA
Akizungumza na Nipashe kuhusu barua anayodaiwa kuiandika kwenda kwa walimu wakuu wa manispaa yake kuhusiana na makato ya Sh. 1,500 kwa kila mwanafunzi, Shemwelekwa alianza kwa kukiri kuandika barua hiyo, lakini akakataa kutoa maelezo zaidi kwa madai kwamba anayepaswa kuulizwa ni mkurugenzi wa manispaa yake.
"Siwezi kuzungumza na wewe. Ukitaka maelezo zaidi nenda kamuulize Mkurugenzi wa Manispaa,'' alisema Shemwelekwa.
Hata hivyo, alipoulizwa, Mkurugenzi wa manispaa hiyo anayetajwa kwa jina la Kagurumjuli Titus, alisema (yeye) hana taarifa ya kuandikwa kwa barua hiyo ambayo Nipashe inayo nakala yake.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisema kama walimu wakuu hawakuridhika na barua iliyowataka kukata fedha hizo kwa kila mwanafunzi, wangepaswa kufika kwake ili awaweke meza moja na ofisa huyo wa elimu (Shemwelekwa) na kufikia muafaka badala ya kukimbilia kwenye chombo cha habari.
Licha ya mkurugenzi kudai kuwa haijui barua hiyo, nakala mojawapo ambayo Nipashe inayo inaonyesha kuwa miongoni mwa waliotumiwa nakala kwa tarifa ni pamoja na yeye (Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni) na pia Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam.