Jeshi la polisi mkoani Arusha jana lilifanikiwa kumnusuru meneja wa kiwanda cha kutengeneza bidha za plastiki cha Best Pack kilichopo jijini Arusha,Vijay Kumar raia wa India baada ya kunusurika kupigwa na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Katika tukio hilo meneja huyo alifanikiwa kujifungia katika mojawapo ya ofisi kabla ya kuokolewa na polisi ambao walimfikisha katika kituo kikuu cha polisi cha kati na kumhifadhi kabla ya kumwachia kwa sababu za kiusalama
Tukio hilo lilitokea jana katika ofisi za kiwanda hicho zilizopo eneo la Kwa Idd nje kidogo ya jiji la Arusha ambapo wafanyakazi wa kiwanda hicho waligoma kufanya kazi wakipinga kitendo cha kampuni hiyo kutoa tangazo la kusitisha mikataba yao ya ajira kinyume na sheria.
Mbali na madai hayo baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho walilalamikia hatua ya kutoplipwa mishahara yao ya mwezi Machi pamoja na mafao mbalimbali kama malipo ya muda wa saa za ziada pamoja na kiiunua mgongo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho walidai kwamba uongozi wa kiwanda hicho juzi ulibandika tangazo la kusitisha mikataba yao ya ajira katika lango kuu la kuingia kiwandani hapo kinyume na sheria jambo lililowastua.
Catherine Samwel na Babaa Kibori ambao ni watumishi wa kiwanda hicho walisema kwa nyakati tofauti kwamba mnamo machi 17 mwaka huu walifanya kikao na uongozi kujadili malipo yao mbalimbali baada ya uongozi wa kiwanda hicho kutaka kukifunga lakini kikao hicho hakikumaliza kwa suluhu.
Walisema kwamba juzi majira ya asubuhi wakati wanaingia kazini walikuta tangazo likiwataarifu kwamba mikataba yao ya ajira imesitishwa bila taratibu na kanuni jambo lililowapelekea kuvamia ofisi ya meneja huyo wakitaka majibu ya uhakika.
Hatahivyo,wakati wakivamia ofisi ya meneja huyo alijitahidi kukwepa na kisha kujifungia katika mojawapo ya ofisi kiwandani hapo ambapo baada ya muda polisi walifika na kumchomoa kabla ya kumfikisha mbele ya mikono ya jeshi hilo kwa sababu za kiusalama.
Akihojiwa na mtanda huu meneja huyo alisema kwamba uongozi wa kiwanda chao tayari umeshaandaa taratibu za malipo ya mishahara na mafao mbalimbali kwa watumisho hao na watakwenda kuwalipa watumishi hao wiki hii.
Meneja huyo alifafanua kwamba wameamua kusitisha mikataba ya ajira kwa watumishi hao kutokana na kampuni hiyo kutozalisha kwa faida lakini watazingatia taratibu zote za kusitisha mikataba hiyo.