Rais Magufuli Afichua Vietnam ilivyopaa Kiuchumi Kwa Mbegu za Tanzania..

Rais Dk. John Magufuli amefichua siri kwamba mbegu za mpunga, korosho na samaki kutoka Tanzania ndivyo vilivyoipaisha Vietnam Kiuchumi.

Amesema mbegu hizo zilizochukuliwa miaka ya 1970, zimeifanya nchi hiyo kuwa kinara katika uzalishaji wa mazao hayo pamoja na ufugaji wa samaki.

Kutokana na maendeleo hayo, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuiga Vietnam katika uzalishaji wa mpunga, korosho na ufugaji wa samaki, ili kuchangia uchumi wa nchi na pato la taifa.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam alipofanya mazungumzo na Rais wa Vietnam, Truong Tan Sang, ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi.

Alisema Watanzania wanatakiwa kuiga Vietnam yenye watu wanaokadiriwa kuwa milioni 91, ambao wamepiga hatua kubwa ya uzalishaji, hata uchumi wao umekua kwa asilimia 50.

Rais Magufuli aliongeza kuwa Vietnam imefanikiwa kupunguza umasikini kwa asilimia 50 na sasa imetoka katika uchumi wa chini hadi uchumi wa kati.

Alisema nchi hiyo ilichukua mbegu za korosho na mpunga nchini pamoja na samaki katika Ziwa Victoria na kuwapeleka kwao, lakini kwa sasa ni vinara wa uzalishaji wa mazao hayo, huku Tanzania ikiwa haijapiga hatua yoyote.

Alisema Tanzania ina mifugo milioni 22 na ni nchi ya pili kuwa na idadi kubwa ya mifugo Afrika, ya kwanza ikiwa Ethiopia lakini Tanzania haizalishi bidhaa ya ngozi kwa wingi.

Rais Magufuli alisema hiyo ni changamoto kubwa kwa Tanzania kuhakikisha inapiga hatua na kwamba ujio wa Rais Tan Sang utasaidia kuweka uhusiano karibu katika kibiashara, uwekezaji, mawasiliano na kilimo.

“Vietnam wanazalisha mpunga mara tatu kwa mwaka, lakini sisi tunazalisha mara moja. Walikuja kuchukua mbegu ya samaki wa maji baridi miaka ya nyuma, lakini sasa wanaongoza kwa ufugaji duniani,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema wafanyabiashara wasione taabu kujifunza kwa Vietnam kwa kuwa imeobobea katika kilimo kwa sasa, japokuwa walijifunza kutoka Tanzania.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli alisema biashara yenye thamani ya dola za Marekani milioni 300 (Sh. bilioni 640) imefanyika kati ya Tanzania na Vietnam.

Kutokana na mafanikio hayo, serikali za nchi hizo zimekubaliana kuongeza biashara hiyo hadi kufikia dola bilioni moja (zaidi ya Sh. trilioni mbili).

Naye Rais Tan Sang alisema Tanzania ni moja ya nchi za mwanzo zilizokuwa na uhusiano wa kisiasa wa karibu na Vietnam miaka ya 1960.

Alisema Tanzania ni nchi iliyopiga hatua katika uchumi barani Afrika, hivyo watashirikiana katika biashara, uwekezaji, mawasiliano na kilimo.

Wakati huo huo, Rais Tan Sang alitembelea  ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam  na kupokewa na Mwenyekiti wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

“TANU ndiyo ilikuwa inaisaidia Vietnam katika kudai uhuru, tena nakumbuka vijana wa TANU wakiongozwa na Benjamini Mkapa (Rais mstaafu) walichangisha pesa kwa ajili ya kukisaidia chama hicho,” alisema Kikwete.

Kikwete alisema uhusiano wa Tanzania na Vietnam ulianza zamani wakati TANU na Chama cha Kikomonisti cha Vietnam viliposhirikiana katika mapambano ya kudai uhuru.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad