Rais John Magufuli jana aliitaja kampuni ya kuzalisha umeme ya IPTL wakati akizungumzia matatizo yanayosababishwa na kununua umeme unaozalishwa na mitambo ya kukodi na kupiga marufuku mikataba hiyo.
Rais pia alipuuzia shutuma zinazorushwa dhidi ya Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana na sakata la IPTL, akisema “wakati mwingine vitu vizuri hupigwa vita” na hivyo amemrejesha mbunge huyo wa Musoma Vijijini kwenye wizara hiyo kwa sababu ya uchapakazi na si siasa.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akifichua kashfa za ufisadi ambazo hazikuwahi kujadiliwa vikali katika utawala uliopita, lakini jana alitoa mfano wa IPTL kama moja ya mikataba iliyoisababishia Serikali matatizo.
Kashfa zilizoikumba sekta hiyo ni pamoja na mkataba wa uzalishaji umeme na kampuni ya Richmond Development iliyodhihirika baadaye kuwa haikuwa na uwezo, uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyohusisha IPTL, mikataba ya ununuzi umeme kwa bei kubwa kutoka kampuni binafsi na ununuzi wa umeme kutoka mitambo ya kukodi.
“Ni matumani yangu kuwa sitasikia tena mnaleta mapendekezo kwamba tunataka kuongeza mkataba huu au tunataka kukodi mtambo huu.Suala la kukodi likalegee, lizimie na life kabisa huko,” alisema Rais Magufuli wakati akizindua ujenzi wa kituo cha umeme cha mradi wa Kinyerezi ll utakaokuwa ukizalisha megawati 280 kwa mwaka jijini Dar es Salaam jana.
“Hayo mawazo yafe, sasa tuwe na mawazo ya kujenga mitambo yetu. Cha kuazima ni kibaya. Hivi sasa vya kukodi na vya kuazima achaneni navyo. Nendeni na mawazo ya kujenga mitambo yetu.
“Tumechoka kuchezewa. Kuna miradi hapa ya hovyo kweli. Kila siku inazaa matatizo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri (Muhongo) lisimamie hilo. " Alisema Rais Magufuli
Alisema Profesa Muhongo akipata ushauri kutoka kwa wataalamu wake kuhusu miradi ya kukodi mitambo, atambue kuwa hawafai. “Ujue huyo si mtaalamu mzuri, ikiwezekana mtoe. Wataalamu wako wakuletee mawazo ya kujenga mitambo yetu,” alisema.
Rais Magufuli alisema ni lazima ufike wakati Tanzania iwe na umeme wa uhakika tena wa kujitegemea.
“Si umeme kwa kukodisha- kodisha. Umeme ni wa kutumia watu. Na ndiyo maana kumekuwa na matatizo mengi. Mara IPTL mara nini. Ni kwa sababu tulizoea umeme wa kukodisha kwa wafanyabiashara,” alisema.
Kampuni ya IPTL iliingia kwenye mgogoro na Serikali baada ya kudaiwa kuwa inaitoza Tanesco tozo kubwa gharama za uwekezaji kuliko makubaliano ya mkataba.
Wakati wa kashfa ya escrow, zaidi ya Sh300 bilioni zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti hiyo kusubiri kumalizika kwa mgogoro wa kimkataba baina ya IPTL na Tanesco zilichotwa na kuonekana zikiingia kwenye akaunti za mawaziri, majaji, wabunge na watumishi waandamizi wa Serikali, jambo lililolifanya Bunge limlazimishe Profesa Muhongo awajibike kwa kushindwa kusimamia fedha za Serikali.
Profesa Muhongo alijiuzulu, lakini akateuliwa na Rais Magufuli kurudi kwenye nafasi hiyo na jana mkuu huyo wa nchi hakusita kummwagia sifa.
“Wizara ya Nishati mmenifurahisha sana. Tuachane na mitambo ya kukodi. Tumechoka kufanya biashara na wawekezaji wa ajabu ajabu. Halafu tunalipia capacity charges za ajabu na umeme unakuwa juu. Tunawapa shida Watanzania wa maisha ya chini,” alisema Magufuli.
“Nendeni kwa kasi ya hapa kazi tu. Na ndiyo maana niliamua kumrudisha Profesa Muhongo hapo. Wakati mwingine vitu vizuri vinapigwa vita. Sichagui mwanasiasa. Mimi nataka mtu mchapa kazi. Maendeleo hayana chama.”
Akizungumzia ujenzi wa kituo cha Kinyerezi ll utakaogharimu dola 344 za Marekani (sawa na Sh688 bilioni), Rais alisema amefarijika kuona ndani ya muda wake mfupi akiwa madarakani amealikwa kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo.
Alisema Serikali ya Japan ilitoa dola 292 milioni za Marekani na Tanzania ilitakiwa kutoa dola 52 milioni za Marekani sawa na asilimia 15, lakini ikashindikana na kutakiwa wasubiri.
“Baada ya makusanyo kuimarika tulipoingia madarakani mwezi Novemba na Desemba mwaka jana, tulitoa maelekezo na hizo dola 52 milioni sawa Sh110 bilioni za Tanzania na zikapatikana ndiyo maana leo tupo hapa kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi huu kuanza,” alisema.
“Hivi sasa tuna uwezo wa kuzalisha megawati 1,200 hadi 1,500 za umeme kwa mwaka. Sasa tumefikia 1026. Hiyo ina maana kuwa kila Mtanzania kwa sasa anatumia wastani wa wati 30 kwa mwaka,” alisema.
Pia alisema amefurahi kupata taarifa kuwa mradi ya Kinyerezi l utaongezewa uwezo wa uzalishaji kutoka megawati 150 hadi 335.
“Nimeambiwa mkandarasi anataka dola 20 milioni za Marekani (sawa na Sh 40 bilioni). Sasa kama tuliweza kutoa hela kwa ajili ya Kinyerezi II, hatuwezi kushindwa kuongeza kwa ajili ya Kinyerezi l. Hiyo hela tutatafuta hata mwezi huu tutampa,” alisema.
Rais Magufuli Akerwa Na Mikataba Mibovu Ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL....Aeleza Kilichomfanya Amrudishe Profesa Muhongo Wizara ya Nishati
1
March 17, 2016
Tags
Sawa kabisa Raisi wetu mpendwa. Yaani serikali ile iliyopita ilikuwa Korrupt mpaka. Mawaziri wakajigawia mahela ya walala hoi wanayotozwa. Kwa kuzimisha naa soo wakaona wawape na majaji mbuzi wenzao wapumbavu kama wao. Hao majaji mbuzi hawana ujaji wala nini nao wamejaa na kunuka rushwa. Dhurumaa. Wanajipa laaana tu wenyewe kwa rushwa na dhrumaa.
ReplyDelete