Udhaifu wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete inaelezwa ilikuwa ni uzito katika kufanya uamuzi. Wengi tulichukia jambo hilo. Sasa tumempata John Magufuli Rais wa uamuzi wa haraka.
Ulinganifu mwingine ni jinsi watu walimvyomjadili Magufuli kabla hajawa rais na baada ya kuwa kushika wadhifa huu.
Kama ilivyo ada, enzi ya mkuu wa nchi inapoelekea ukingoni, watu hujadili wanasiasa wanaoweza kumrithi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati kipindi cha Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi (1986 – 1995).
Ilikuwa hivyo pia kipindi cha Rais Mkapa (1995 – 2005) na baadaye pia katika kipindi cha Rais wa Awamu ya Nne, Kikwete (2005 – 2015).
Nakumbuka katika miaka mitano ya mwisho ya Kikwete, mijadala ilianza kuibuka katika vijiwe, ofisini na majukwaa mengine mbalimbali juu ya nani angefaa kumrithi.
Rais wetu wa sasa, Magufuli, naye alikuwa miongoni mwa waliojadiliwa, ingawa hakupewa nafasi kubwa na watu wengi.
Wengi waliomjadili Magufuli walimsifu, pia walitaja upungufu waliodhani kuwa wangemfanya asifae kushika wadhifa huo.
Licha ya sifa ya kutoa uamuzi wa haraka niliodokeza awali, sifa nyingine nzuri ambazo Magufuli alitajwa kuwa nazo ni utendaji uliotukuka katika historia ya maisha yake ya kisiasa.
Akiwa Waziri wa Ujenzi na kabla ya hapo Waziri wa Uvuvi, Magufuli alijulikana kama mpambanaji aliyesisitiza katika matokeo. Magufuli hakuvumilia makandarasi wazembe na wanaochelewesha kazi na pia alipambana na uvuvi haramu.
Kabla ya kuwa mgombea, wachambuzi pia walimtaja Magufuli kuwa ni msafi na muadilifu, ikilinganishwa na wengine ndani ya CCM na hakuwa na makundi.
Rais Magufuli amebeba sifa hizo katika utawala wake akionyesha mfano wa uchapakazi na kusimamia uadilifu kuanzia siku ya kwanza ya utawala wake na kuambukiza sifa hizo timu yake ya wasaidizi na sasa tunaona wakihangaika huku na kule kumridhisha bosi wao.
Udhaifu aliotajwa kuwa nao
Mijadala ya mrithi wa Kikwete iliibua pia udhaifu wa Magufuli, huku wengi wakisema hafai kuwa kiongozi mkuu yaani mtu wa mwisho katika kutoa uamuzi.
Waliomtathmini waliona Magufuli ni mtu wa maamuzi ya haraka, mwenye misimamo mkali (au mbishi) na wakati mwingine hutawaliwa na mihemko na kushindwa kufikiria vema kabla ya kutoa kauli.
Wakosoaji walisema akiwa mkuu wa nchi, ipo hatari kuwa angeweza kutoa kauli na maamuzi ya jazba na kuishushia heshima nafasi hiyo. Akiwa mtu wa mwisho, kama akitoa uamuzi usio sahihi, angekosekana mtu wa kuingilia kati na kurekebisha.
Wakosoaji walisema nafasi ya urais inahitaji mtu mwenye uwiano mzuri wa ukali, busara na diplomasia kwani wakati fulani katika nchi zetu sheria peke yake haitoshi kutenda haki.
Waliomtathmini Magufuli kipindi kile walisema angeweza kuwa Waziri Mkuu mzuri, lakini siyo nafasi ya urais kwa sababu kutokana na wajihi wake, alihitaji bosi wa kumdhibiti anapovuka mipaka.
Wakosoaji pia walisema Magufuli ana sifa ya utendaji kuliko uongozi. Walipozungumzia kiongozi walimaanisha mtu mwenye dira ajuaye wapi anataka kuipeleka nchi, mwenye uelewa mpana wa falsafa, itikadi na mwelekeo wa siasa za ulimwengu huu wa leo.
Kutokana na taaluma yake ya sayansi, Magufuli alifahamika kwa ubobezi wake wa vitu vya kiufundi vya Wizara za Ujenzi na kabla ya hapo Wizara ya Mifugo ikiwamo kuhifadhi takwimu mbalimbali.
Mifano iliyotolewa
Akiwa Waziri katika Wizara ya Ujenzi, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kuweka alama ya ‘X’ kwenye nyumba zilizojengwa katika maeneo ya hifadhi ya barabara na kuagiza wahusika wabomoe.
Waathirika walilalamika kwa rais na kudai hawakujua ni eneo la hifadhi ya barabara na kuhoji kwa nini Serikali haikuwazuia wakati huo na kuwaacha wakijenga nyumba na kuishi miaka mingi? Kikwete akaamua kusimamisha zoezi hilo.
Mfano mwingine ni mgomo wa wenye malori ya mizigo ulioanza baada ya Magufuli kuagiza watozwe asilimia tano kwa kila lori litakalozidisha mizigo, kwa mujibu wa sheria. Mgomo huo uliendelea kwa siku kadhaa na kusababisha hasara kubwa kwa pande zote ndipo Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda, akaingilia kati na kusitisha tozo hiyo.
Matukio hayo mawili yalionyesha kuwa Magufuli ni mtu wa misimamo na mtendaji anayefuata sheria hadi nukta.
Hata hivyo, wakati fulani busara za kisiasa huhitajika. Angekuwa rais, huenda Magufuli angeng’ang’ania misimamo yake mikali na kuleta zaidi madhara kisiasa na kiuchumi.
Magufuli pia alituhumiwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh1 trilioni katika kesi ya meli ya Wachina waliokamatwa mwaka 2009 kwa tuhuma za uvuvi haramu.
Baada ya mchakato mrefu, mahakama iliagiza Serikali kulipa watuhumiwa meli, samaki waliokuwamo na gharama za mawakili.
Meli hiyo ilikamatwa wakati Magufuli akiwa Waziri wa Uvuvi kuanzia 2008 – 2010 kabla kuhamishiwa Wizara ya Ujenzi.
Huu ulitajwa kuwa ni mfano wa maamuzi yaliyokosa umakini kutokana na jazba. Vilevile, wakosoaji wa wakati ule pia walitaja kauli tata na za kuudhi za Magufuli ikiwamo aliyoitoa kwa wakazi wa Kigamboni kuwa wapige mbizi kama hawataki kulipa nauli mpya ya kivuko!
Magufuli baada urais
Je, yale yaliyoonekana kuwa ni udhaifu wa Magufuli yamethibitika baada ya kuingia madarakani? Hili ni swali muhimu ambalo wachambuzi waliojadili siku 100 za Rais Magufuli wangetusaidia kutathmini.
Kwa mtazamo wangu, Magufuli hajabadilika, alivyokuwa ndivyo alivyo. Yaliyodhaniwa kuwa ni upungufu wake, yamethibitika katika kipindi ambacho ameiongoza nchi.
Bomoabomoa iliyositishwa na Rais mstaafu Kikwete, ilianza tena baada ya Magufuli kuingia madarakani. Kujali utu ndiyo sababu iliyomsukuma Kikwete kusimamisha kazi hiyo. Ni jambo zuri kuwa Serikali ya Rais Magufuli iligundua ugumu wa utekelezaji wa zoezi hilo na gharama zake kisiasa na kuamua kulisimamisha kiaina.
Hii inaonyesha inawezekana kupata busara akiwa kazini.
Kwa sasa mambo mengi yanaendelea nchini. ‘Majipu’ yanatumbuliwa. Nyuma ya hadithi za hayo majipu kuna heshima za watu wenye familia zao zimewekwa rehani. Serikali ikikosea kipimo kwa kutumbua uvimbe kwa kudhani ni jipu, hatari yake ni kubwa. Pia, ikitumbua majipu vibaya mgonjwa anaweza kudhurika badala ya kupona.
Hata hivyo, katika siku zijazo yafaa Rais Magufuli awe muangalifu zaidi na kuzingatia kuwa taasisi anayoingoza ni kuu, yenye heshima huku yeye akiwa mtu wa mwisho kwa uamuzi.
Siku aliyotangaza baraza lake la mawaziri, Rais Magufuli alijibu maswali ya waandishi wa habari kwa mkato na kudhihirisha upungufu wa waandishi.
Kadhalika, wakati anaongea katika siku ya kilele cha sheria duniani, Rais Magufuli aliahidi kutoa robo ya fedha ambazo mahakama ingeziokoa kutokana na kesi za waliokwepa kulipa kodi, kesi ambazo Serikali yenyewe ndiyo mdai. Wadaiwa watatendewa haki?
Vilevile, akiongea na wazee wa Dar es Salaam, Magufuli aling’aka kuwa kamwe hataingilia kati mgogoro wa Zanzibar kwa sababu anaheshimu sheria na uhuru wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kwamba wasioridhika waende mahakamani.
Tulitegemea matamshi haya yangetolewa na Katibu Mkuu wa CCM na Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Balozi Seif Idd.
Kauli hii ikiwa imetoka kwa Magufuli, mtu wa mwisho katika uamuzi ya kiserikali. Yako wapi matumaini ya kupatikana suluhu Zanzibar? Ni muhimu kwa Magufuli awe muangalifu na maagizo mbalimbali anayoyatoa kuepuka kukiuka sheria, maadili ya uongozi au kusababisha madhara kutokana na matokeo yasiyotarajiwa.
Hivi karibuni, Magufuli alizuia uagizaji wa sukari ila kwa kibali maalumu, hatua ambayo inatajwa kupandisha bei ya sukari. Katika suala la dira, hivi karibuni, msomi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo akitathmini siku 100 za Rais Magufuli alimkosoa kwa kusema bado hajaona dira ya kiongozi huyo, akitoa mifano ya sera za kiuchumi. Nakubaliana naye.
Kinachotokea sasa katika utendaji wa Rais Magufuli ni kama mzazi ambaye mwanaye yu mgonjwa anahangaika apone. Dira ya kimalezi ya mtoto huyu imesahauliwa.
yotebyamesababishwa na kiongozi mwenye tamaa ya fedha, mwenye matumizi ya anasa na fisadi mkubwa alie maliza kipindi chake kamwachia nchi mwenzie ina hali mbaya sana
ReplyDeleteDah aiseee!! Huyu mwandishi ni mtu wa hovyo sana kama ilivyo kwa watu wengine wanao ona mapungufu ya JPM badala ya kuyaangalia yale mambo ambayo ni mazuri anayoifanyia Nchi. Huyu mwandashi ameshindwa kufanya uwiano wa habari yake dhidi ya namna ambavyo hiyo Nchi ambavyo imekuwa ikiliwa na wajanja huku wananchi wengi wao wakidhalilika kwa hali mbaya ya umaskini uliokithiri. Hilo suala la Dira sijui dira ni jambo ambalo tumekuwa tukilisikia na kuliona katika hizo awamu zilizopita, sasa swali la kujiuliza je huo mfumo wa hizo dira hewa umeifikisha wapi Nchii????? Je wananchi walinufaika nini na hizo dira mnazokaa kutueleza kila kukichaaa?????? Pamoja na Nchi kuongozwa na hizo dira mbona wewe mwandishi hutuelezi ni kwa nini ma kontena yalikuwa yanaibiwa na kwa nini bomba la mafuta lilikuwa halina mita za kusoma hayo mafuta???? Acheni dhihaka kwa watanzania nyie waandishi uchwara eti kwa sababu tu mna hiyo access ya kuwasilisha mawazo yenu ambayo feki kwa wananchi.
DeleteKIZURI HAKIKOSI KASORO,HATA MAGUFULI HAWEZI KUKOSA KASORO,ILA TUFIKIE MAHALI TUKUBALI KASORO NI NDOGO(CHACHE)SANA KULIKO MAZURI.MAGUFULI ADUMU TUU.
ReplyDeleteJipu
ReplyDeleteSemeni,imbeni,lakini ukweli utabaki kuwa Magufuli anakaribia kuwa na sifa za kiongozi anaetakiwa TZ kwa hapa ilipofikia.
ReplyDeleteMungu wetu tunakuomba endelea kumpa hekina na ulinzi JPJM.
All the best JPM
ReplyDeletemagufuli amekuja muda muafaka
ReplyDeletena apo alipo ndio panamfaa
ile meli ni uhuni magufuli alichezewa lkn ukweli ni kwamba ilikuwa na makosa
viongozi wa ccm wanajua ilo
Mungu akulinde rais wetu JPJM
umebwabwaja tu mwandishi huna hoja yenye mashiko, nyie ndio wale wale ant-magufuli
ReplyDeletehakuna kam JPJM kwa sasa
ReplyDeleteNchi hii ilishaoza kabisa. Makala haya yameoza vile vile. Mwandishi wa haya makala akili yake imeoza vile vile. Nchi ilifikia pabaya ilihitaji mzalendo wa kweli asiekuwa na favor na mtu au fear katika kusimamia sheria na kuchunga rasilimali za nchi kwa manufaa ya watanzania wote, kuja kwa Magufuli kama bahati kwa watanzania. Hao waliomtathmini Magufuli kabla ya kuwa raisi na kutoa tathmini za kifisadi zidi yake ni majipu ambayo yalikuwa yakimuhofia yakwamba kama mueshimiwa magufuli atakuwa raisi basi wale wachache waliokuwa wakiitafuna hii nchi wakijinufahisha wao kwa wao watakiona kiama chao na ndicho kilichotokea na kinachoendelea hivi sasa. Sasa wamebakia kutoa makala pumba za majungu kama kawaida yetu watanzania badala ya kutoa makala ya kuwaelimisha watanzania juu ya dhamira nzuri na safi ya Muheshimiwa Maghufuli ya kuhakikisha watanzania na Tanzania wanaondokana na umasikini kwani uwezo upo,uongozi mzuri upo,rasilimali zipo za kutosha sasa kipi kitakachoizua Tanzania kutoka? Magufuli hafanyi kazi kwa kumkomoa mtu wala hafanyi kazi kwa kutaka sifa.Maghufuli ameamua kujitolea mhanga katika kuwatumikia watanzania kuwaondolea kero zao na kuliondosha taifa katika janga la umasikini katika nchi iliojaa rasilimali za kutosha. La msingi zaidi katika historia ya nchi zote zilizopiga hatua za kimaendeleo duniani zilifanya hivyo baada ya kubahatika kupata viongozi wenye misimamo mikali ya uwajibikaji wa kalba ya Magufuli na kuweka misingi imara. Na kama watanzania watampa muheshimiwa Maghufuli ushirikiano wa kweli na kuweka mbele uzalendo basi faida yake wataiona muda si mrefu. Mfano mmoja tu ambao naweza kuutowa ni faini ama adhabu zinazotozwa kwa wanaoegesha magari katika wakati sio na mahala sipo kwa hapa New York city basi pesa zake zinauwezo wa kuendesha shuguli za maendeleo katika majimbo mengine masikini hapa marekani. Na ole wake mtu apewe adhabu halafu asilipe unaweza kujikuta unaishia jela na vile vile kuiweka driving licence yako katika twasira mbaya.Sasa leo ati mtu anafika mpaka kujenga katika eneo la bara bara kinyume cha sheria halafu akabembelezwe katika kuvunja nyumba yake jamani? Sasa hapo kuna serikali au masihara ya serikali? Cha kufanya kwa watanzania ni kumuomba mueshimiwa magufuli azidishe bidii na ashikilie uzi huo huo ikiwezekana azidishe ukali na Mungu atamsaidia kwa hayo majungu yasokuwa na mshiko ni sawa kelele za chura mtoni haziwezi kuzuia watu kutumia maji.
ReplyDelete