Hali bado tete! Baada ya Gazeti la Ijumaa Wikienda ambalo ni dugu wa damu na hili toleo la Jumatatu iliyopita kutoka na habari yenye kichwa kisemacho; WASTARA ATOROSHWA HOSPITALINI, habari mpya ni kwamba, nduguze wameshindwa kujua wapi alipo mpaka sasa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Ijumaa iliyopita, baadhi ya ndugu wa Wastara, wakiwemo dada zake, waishio jijini Dar walikodi gari ndogo ili kwenda Morogoro kumfuata Wastara na kumrejesha Dar ambako ndiko kwenye makazi yake, lakini walidunda dakika za mwisho wakiwa Mwenge, tayari kwa safari.
HIKI HAPA CHANZO
“Jamani Wastara amezua balaa. Mnajua kwamba ndugu hatujui alipo mpaka sasa. Baada ya kuondoka nyumbani kwa mumewe (Mbunge wa Jimbo la Donge, Zanzibar, Sadifa Juma) hapa Dar, alikwenda Morogoro kwa huyo mtu aliyesema ni babu yake, Abdulaaziz Babu kwa lengo la kupumzisha akili.
“Sasa baada ya kusikia ameugua ghafla maradhi ya kisukari na moyo na amelazwa Hospitali ya St. Herry Health Centre , sisi ndugu tuliamua kumfuata. Sasa tukiwa ndani ya gari, tulipofika Mwenge, tukampigia simu Wastara ili kumjulisha kwamba tunakwenda.
“Alichotujibu sasa. Alimwambia dada yetu mkubwa kwamba, kama tunataka kumkosa maisha yetu yote tumfuate, la sivyo tusiende Morogoro. Yaani alimaanisha kwamba, tukimfuata anaweza kujiua. Akasema atakuja mwenyewe na atafikia kwa huyo dada yetu mkubwa.
“Sasa ile ilikuwa Ijumaa iliyopita. Mpaka sasa tunavyoongea (juzi Jumanne), hajaja na mbaya zaidi tukipiga simu hapokei, hajibu meseji. Yule babu tumempigia simu akasema Wastara alimtoa hospitali na kwenda kumpangia chumba hotelini, sasa sisi hatujui anakoishi kule Morogoro na wala hiyo hoteli aliyompeleka ni ipi,” alisema ndugu huyo.
Baada ya maelezo hayo, juzi, Amani lilimwendea hewani Wastara ambapo simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa. Baadaye ikawa haipatikani.
Baadaye Amani lilimpigia babu huyo ambapo alisema;
“Wastara yupo fiti sasa, lakini huwezi kumpata kwenye simu kwa sababu ya mambo yaliyojitokeza hivi karibuni.”…
Ndoa ya Wastara na Sadifa ilidaiwa kuvunjika rasmi Machi 21, mwaka huu baada ya kuishi kwa siku 74 tangu kufungwa kwake, Januari 22, mwaka huu huko Tabata jijini Dar.
Hata hivyo, Sadifa akielezea kuhusu madai ya kuvunjika kwa ndoa yake alipozungumza na Magazeti Pendwa ya Global wiki iliyopita, alisema yeye hajatoa talaka huku akimshangaa mtu anayejiita ni babu wa Wastara kuzungumza kwenye vyombo vya habari kwamba, Wastara amepewa talaka mbili.
Kwa upande wake, Wastara alipozu- ngumza na Magazeti Pendwa alikiri kupewa talaka.
Chanzo: GPL