Serikali ya Tanzania imetoa tamko kuwa kwa sasa haina mpango wowote wa kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa ambayo yametokana na vitendo vya ujangili na vifo asilia vya tembo.
Tamko hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress alipotembelewa na balozi huyo ofisini kwake kujadili maendeleo ya sekta ya Maliasili mchini.
Prof. Maghembe alisema hayo baada Balozi huyo wa Marekani hapa nchini kutoa pendekezo kwa Serikali ya Tanzania kuchoma sehemu meno ya tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu ya dhamira ya Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.
"Naomba niweke wazi kuwa kwa sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya, tunaweza kuyatumia kwenye tafiti za kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za ujangili ambazo zipo mahakamani na nyingine ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi" Alisema Prof. Maghembe.
Zipo nchi mbalimbali duniani ambazo zimechukua hatua ya kuteketeza meno yake ya tembo yaliyohifadhiwa ikiwemo nchi jirani ya Kenya na Malawi ambapo inaaminika kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kushawishi Ulimwengu kukomesha biashara hii haramu ya meno ya tembo.
Nchi nyingine ni Chad, Ubelgiji, Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno. Kwa upande wa nchi ambazo zina msimamo sawa na Tanzania katika kuendelea kuhifadhi meno yake ya Tembo ni pamoja na Afrika ya Kusini, Botswana na Zimbabwe.
Akizungumzia kuhusu kuendeleza sekta ya Maliasili nchini, Prof.Maghembe amemuomba Balozi wa Marekani Bw. Mark Childress kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta hiyo kwa kuleta wawekezaji mbalimbali kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia kwenye mapambano dhidi ya Ujangili.
Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za kisasa na kuendeleza vivutio mbalimbali vilivyomo hapa nchini.
Prof. Maghembe amemshukuru balozi huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali ya Marekani ya kuendeleza sekta ya Maliasili nchini ukiwemo wa hivi karibuni wa mbwa maalum (Snifer Dogs) kwa ajili ya kusaidia utambuzi wa rasilimali za Maliasili zinazoweza kutoroshwa nje ya nchi kupitia bandari na viwanja vya ndege.
Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao baina ya Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali ya Marekani imetoa misaada mbalimbali ambayo jumla yake ni dola za kimarekani Milioni 41.35 katika kusaidia eneo la uhifadhi hapa nchini.
Akizungumzia mahusiano baina ya Tanzania na Marekani Balozi Mark Childress alimueleza Prof. maghembe kuwa Serikali ya Marekani itaendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ambapo pia ofisi yake ya ubalozi imeshatafuta wadau mbalimbali ambao wapo tayari kusaidia fedha, vifaa na mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na mapambano dhidi ya ujangili.