Kitendawili cha nani atavaa viatu vya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, aliyeshika wadhifa huo kwa miaka 11, kitateguliwa leo jijini hapa baada ya kikao cha Baraza Kuu la chama hicho, lakini tayari sifa na udhaifu wa majina yanayopewa nafasi kubwa vimewekwa hadharani.
Wanaotajwa kuwa na sifa ya kurithi nafasi ya Dk. Slaa ni waliokuwa wasaidizi wake wa karibu Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.
Vikao vya Kamati Kuu vinaendelea jijini Mwanza kuandaa agenda za Baraza Kuu ambalo litakutana leo kwa ajili ya kujadili majina mawili ambayo yatawasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya chama hicho vinaeleza kuwa Mnyika ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kibamba huenda asifikiriwe sana katika nafsi hiyo kutokana na ukaribu wake na Dk. Slaa.
Imeelezwa kuwa hata Dk. Slaa alipotangaza kuachana na siasa, Mnyika hakuonekana katika majukwaa na vikao mbalimbali ikiwemo kikao cha Kamati Kuu, kilichopitisha jina la Edward Lowassa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa 2015.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema Mwalimu hawezi kuvaa viatu vya Dk. Slaa licha ya kufanya naye kazi tangu mwaka 2014 hadi Oktoba 2015, kwani licha ya kukaimu nafasi hiyo hakuweza kuendesha chama kama mtendaji mkuu kwa kiwango kilichotarajiwa.
Wachambuzi hao wanasema Mnyika na Mwalimu moja kwa moja wanapoteza imani ya wajumbe wa Baraza Kuu na hata Mwenyekiti akipeleka majina yao, kuna uwezekano wa kukataliwa kwani Katiba inawaruhusu kufanya hivyo.
Mwingine anayeonekana anaweza kuvaa viatu vya Dk. Slaa ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye pia ni mwanasheria wa chama.
Lissu anaelezewa kuwa amekitumikia chama hicho kwa uaminifu, kujitoa kwa muda mrefu kwa nguvu zote bila kujali maslahi anayoyapata na hajaonyesha dalili za usaliti.
Lakini Lissu anatajwa kuwa anapungukiwa sifa kutokana na kuwa na maamuzi ya haraka kwa mambo mbalimbali.
Mwingine anayejadiliwa miongoni mwa wavaaji wa viatu vya Dk. Slaa ni aliyegombea ubunge jimbo la Morogoro Mjini, Marcossy Albany, ambaye ana faida ya kufuta dhana kwamba chama hicho kinaongozwa na viongozi kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini.
Mratibu wa chama hicho Kanda ya Ziwa, Robert Bujiku, naye anatajwa tajwa ikiwa ni mkakati wa kuongeza misuli ya chama kwa kanda ya ziwa.
Mwanachama mwingine anayetajwa ni Fredreck Sumaye, ambaye sifa yake kuu ni kujitoa kuingia upinzani bila kujali atakachopata na alitembea kwenye kampeni nchi nzima kumpigania aliyekuwa mgombea urais aliyekuwa akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wannachi ( Ukawa), Edward Lowasa.
Sifa nyingine ya Sumaye ni kwamba hana makundi na hana tuhuma za ufisadi, lakini wakati vikao hivi vinaendekea Sumaye yupo nchini India kwa matibabu.
"Unajua Mwenyekiti amepewa mamlaka na Katiba ya kupendekeza majina mawili kwenye Baraza Kuu ambalo lina hiyari ya kukubali au kukataa majina husika, hadi sasa ni siri kubwa kwa Mwenyekiti hadi leo atakapotamka majina ya waliopendekezwa," kilisema chanzo chetu na kuongeza:
"Dk. Slaa alikuwa na misuli ndani ya chama, alikijenga kwa muda mrefu hadi ngazi ya chini, wengi wa wanachama wetu wameingia na kumkuta Dk. Slaa hivyo kwa sasa kupata mtu mpya ambaye atavaa viatu vyake siyo jambo jepesi.
"Ni lazima kufanya upembezi kuona mtu makini, mvumilivu, mwenye bidii ambaye atakuwa daraja na mwenye uzoefu katika suasa."
Baadhi ya wanachama na viongozi waliozungumza na Nipashe, walieleza sifa wanazoona zitafaa kwa mrithi wa Dk. Slaa kuwa ni uvumilivu na kufuata nyayo za mtangulizi wake kwa kuwa tayari kubeba lawama na kukijenga chama katika misingi inayotakiwa.
"Chama chenyewe kina taratibu zake, miongozo yake, kanuni, Katiba na sifa hivyo ndiyo hufuatwa katika kumpata kiongozi wa nafasi hiyo," alisema Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Profesa Baregu na kutaja sifa anazoona zinafaa kuwa ni:
“Moja, awe mwenye uelewa mpana siyo anajua mambo ya Chadema tu, bali vyama vingine na kwenye uwanja wa siasa kwa ujumla akiwa na uzoefu mpana na mvumilivu kwa kuwa madonge ya kiasiasa yanayotupwa mengi yanaelekezwa kwa Katibu Mkuu.”