Siri ya Utoroshaji wa Wanyama na Wadudu Hai Kutoka Tanzania Kwenda Nje ya Nchi Imebainika.

Siri ya utoroshaji wa wanyama na wadudu hai kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi imebainika. Wamekuwa wakitumika katika nchi mbalimbali kwenye utafiti, mapambo na kitoweo.

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wetu, umebaini matumizi hayo na kuwa wanyama wanaotakiwa kwa wingi ni mijusi ya bluu, kenge na tumbili wanaopelekwa katika nchi za Ulaya kupitia viwanja viwili vya ndege hapa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Herman Keraryo alisema mbali na wanyama hao, wengine wanaopelekwa nje ni jamii ya nyani, wadudu na ndege.

Alisema hakuna nchi ambayo imejitambulisha kipeke kununua wanyama hao, bali imekuwa ni biashara kati ya mzawa na mnunuzi.

Alipoulizwa kuhusu uhalali wa biashara hiyo, Keraryo alisema mfanyabiashara lazima awe na leseni inayotambuliwa na Serikali; “... na siyo kila ndege anasafirishwa au nyani, kuna aina ya ndege wasioruhusiwa ila kwa kutozingatia sheria, baadhi ya watu wanaivunja.” Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Tanapa, Gerald Bigurube alisema wanyama kama kobe na kakakuona nao wamekuwa wakisafirishwa zaidi kwenda Vietinam na China kwa matumizi ya chakula na dawa.

Alisema matumizi mengine ya wanyama hao wanaopelekwa Marekani na Ulaya yamekuwa ni kwa ajili ya shughuli za mapambo.

“Wanyama hai na wadudu kwa kifupi wana soko pana sana duniani na matumizi yake ni kama hayo lakini inakuwa vigumu kujua moja kwa moja wanapelekwa nchi gani,” alisema.

Bigurube alisema wanyama wengine wamekuwa wakipelekwa kwenye maeneo ya mafunzo ili watu wengine duniani wajifunze historia yao. Imeelezwa kuwa mijusi ya bluu ambayo inapatikana Tanzania pekee ndiyo inayotafutwa zaidi na kila mmoja umekuwa ukiuzwa kwa Euro 5,000 (Sh12.2 milioni.)

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ndani ya Idara ya Wanyamapori, wimbi la ukamataji na utoroshaji wa mijusi hiyo na tumbili linatokana na kuhitajika katika nchi mbalimbali kwa ajili ya utafiti.

“Kitu kinachoibwa zaidi sasa hivi nchini ni hao tumbili kwa sababu wanatumika sana huko nje kwa ajili ya utafiti wa kitabibu,” kilidokeza chanzo chetu na kuongeza: “Hata unavyoona, faru wanauawa ni kwamba wenzetu huko nchi za Asia wanaamini unga wake unasaidia kuongeza nguvu za kiume.”

Matumizi hayo yamebainika siku chache baada ya vyombo vya dola kuwashikilia raia wawili wa Uholanzi kwa kosa la kusafirisha tumbili 61 ambao walikuwa wapelekwe Albania kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

Habari zilizopatikana juzi zilidai kwamba mmoja wa maofisa wanyamapori alipewa bakshishi ya Dola 3,000 za Marekani, sawa na Sh6.4 milioni za Tanzania katika ‘dili’ hiyo ya tumbili 61.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alikiri kuwa tumbili na mijusi hao wa bluu ndiyo wanaowindwa zaidi kwa sasa; “... na huyo Williams Blue Lizard ni mjusi anayepatikana Kimboza na Ruvu. Ndiyo maeneo pekee duniani. Huyo mjusi anakaa juu ya miti kwa hiyo wanachofanya ni kukata mti na kuuangusha ndipo wanawakamata na kuwaweka kwenye mabegi. Wanafanya uharibifu mkubwa.”

Profesa Maghembe alisema mijusi hao huuzwa kati ya Euro 5,000 hadi 6,000 kila mmoja katika nchi za Ulaya.

Kuhusu tumbili, Profesa Maghembe alisema mpango ulikuwa ni kukamata tumbili 441 kwa awamu lakini kikwazo kikubwa kilikuwa ni upatikanaji wa kibali cha kuwasafirisha kwenda nje.

Alipoulizwa kwa nini raia hao wa Uholanzi wamekamatwa wakati walikuwa na kibali, alisema kibali hicho kilitolewa katika mazingira ya rushwa.

“Ni kweli walikuwa na kibali lakini kilitolewaje wakati nilishazuia na waraka ukatolewa? Lakini ujue hawakuwa na kibali pia cha kuwakamata hao wanyama,” alisema.

“Hili jambo lina njama kubwa na ndiyo maana tumeamua lichunguzwe na kile kikosi kazi cha kitaifa ambacho huchunguza makosa makubwa ya kihalifu,” alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad