Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Vyuo vya Ufundi( NACTE),Dr. Primus Nkwera amejiuzulu nafasi yake.
Uamuzi wa kujiuzulu kwa Dr. Nkwera ulitangazwa katika ofisi kuu za Baraza hilo zilizopo Mikocheni Dar es Salaam juzi na Mwenyekiti wa Bodi,Mhandisi Steven Mlote na kusababisha baadhi ya wafanyakazi kuangua kilio.
Akizungumza katika kikao cha dharura cha wafanyakazi wote wa baraza hilo,Mlote alisema Dr. Nkwera amejiuzulu ili kulinda hadhi ya Nacte kutokana na habari iliyoandikwa na Gazeti la Dira ikimtuhumu mambo mbalimbali.
Gazeti hilo la Dira la Jumatatu tarehe 07/03/2016 toleo no.405 lilimtuhumu Katibu Mtendaji wa NACTE, Dr.Primus Nkwera kughushi vyeti vya shahada ya uzamivu baada ya kusomeshwa na serikali Afrika Kusini na kufeli.
Mlote alisema kwa mujibu wa Dr. Nkwera, nafasi hiyo haipaswi kushikwa na mtu mwenye tuhuma ya aina yoyote, na ametafakari na kuona ajiweke kando na uongozi wa Nacte ili uchunguzi ufanyike akiwa pembeni.
"Tumetumia muda mwingi kutafakari hoja ya Dr. Nkwera na hatimaye tumekubali kujiuzulu kwake kwa shingo upande," alisema Mlote na kuongeza:
"Kazi kubwa iliyofanywa na Dr. Nkwera akiwa kiongozi wa Nacte inafahamika na kila mmoja, vilio na machozi ya wafanyakazi wenzake yanadhihirisha kuwa kujiuzulu kwake kunaacha simanzi kubwa.
"Najua mmepata mshtuko mkubwa, lakini Dr Nkwera hajafa, yuko hai na huyu bado ni mtumishi wa serikali. Alichofanya ni kuamua kuachana na ukatibu utendaji.
"Tutaendelea kumtumia itakapobidi kwa ushauri.Wakati mwingine lazima mkubaliane na hali hii, lakini pia endeleen kuchapakazi kwa ufanisi kama kawaida kana kwamba bado mko na Dr. Nkwera."
Kutokana na kujiuzulu kwake, Mlote alisema bodi imemteua Mkurugenzi wa Mitaala wa Nacte, Dr Adolf Rutayunga kukaimu nafasi hiyo wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Dr. Rutayunga alisema viatu alivyoviacha Dr. Nkwera ni vikubwa kwake, lakini akaahidi kuendeleza yote aliyoyaacha.