Walinzi watatu wa Suma JKT na askari mmoja wa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dodoma, wametiwa mbaroni kwa tuhuma za wizi wa kompyuta zinazokadiriwa kufikia 50 mali ya Chuo Kikuu Dodoma (Udom).
Chanzo chetu cha habari kilieleza kuwa wizi huo ulitokea juzi baada ya chuo hicho kufungwa kwa ajili ya mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka.
Inadaiwa kuwa katika wizi huo baadhi ya walinzi wa Suma JKT ambao wanajukumu la kulinda chuo hicho, walihusika huku watatu wakishikiliwa na polisi.
Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa baadhi ya askari wa Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma wanadaiwa kuhusika na kuzua mkanganyiko katika uchunguzi wa tukio hilo.
“Katika wizi huo, pia kuna askari kutoka mjini ametajwa na walinzi wa Suma JKT kuhusika, sasa baada ya kupata taarifa hizo ndiyo wanafanya mpango wa kumkamata,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Ofisa Habari wa Udom, Beatrice Baltazar jana alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba, bado hawajajua idadi kamili ya kompyuta zilizoibiwa.
“Ni kweli kuna wizi wa kompyuta hapa chuoni, lakini sijajua idadi kamili ya kompyuta zilizoibwa, ila kuna walinzi watatu wa Suma JKT wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano,” alisema Beatrice.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa naye alithibitisha kuwapo kwa taarifa za tukio hilo, lakini hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani kwa kuwa yupo likizo.
Hata hivyo, Mambosasa alikanusha kuwa hakuna polisi aliyehusika katika tukio hilo bali ni walinzi wa Suma JKT.
“Hakuna askari wetu aliyehusika katika tukio hilo, wenye jukumu la kulinda chuo hicho ni Suma JKT ndiyo wanaoshikiliwa kwa mahojiano zaidi,” alisema Mambosasa.