Manispaa ya Kigoma Ujiji katika Mkoa wa Kigoma imepewa masaa 24 kupeleka taarifa ya mchanganuo wa fedha iliyopokea kutoka Tamisemi katika bajeti ya mwaka 2014/2015 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi ili kuhakiki matumizi.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, Angela Kairuki baada ya kukagua miradi ya Tasaf na Serikali za mitaa katika Kata ya Majengo, Machinjioni na Kagera zilizopo katika Manispa hiyo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Sekondari ya Kirugu iliyopo Kata ya Machinjioni yaliyojengwa na Tasaf kwa gharama ya shilingi 40 milioni.
Baada ya Shule hiyo kuomba msaada wa kupewa umeme kwa ajili ya kuongeza ari ya wanafunzi kujisomea, ndipo ilibainika shule huyo kupangiwa mgawo wa fedha kiasi cha shilingi 53 milioni kwa ajili ya kuingiza umeme na kujenga matundu ya vyoo ili kuondoa changamoto ya upungufu wa vyoo.
Mkurugenzi msaidizi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Enock Nyanda alisema katika bajeti ya mwaka 2014/2015 Wizara hiyo ilitoa shilingi 2.46 bilioni kwa Halmashauri za Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za Walimu na kuingiza umeme katika Shule za Sekondari.
“Shule hii ya Kirugu ilipangiwa mgawo wa shilingi milioni 53 kwa ajili ya kujenga vyoo na kuingiza umeme, sasa wanapolalamika kwamba hawana umeme na vyoo havitoshi ni jambo linalohitaji ufuatiliaji kuona hiyo fedha iliyotolewa na Wizara ilipelekwa wapi,” alisema Nyanda.
Waziri huyo aliyefuatana na Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya utawala bora na serikali za mitaa alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, John Shauri kuhakikisha taarifa ya mchanganuo wa fedha hiyo unafanyika.
“Tunajua Mkurugenzi wa Manispaa hayupo ana wewe ni Kaimu tu lakini nakuagiza uandae taarifa kamili ya amatumizi yote ya fedha mliyopokea kutoka mgawo huo wa shilingi 2.46 bilioni mueleze nyie Manispaa mlipata kiasi gani na mlizitumiaje, hadi kesho saa tisa mchana muwe tayari mmetuma kwa Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene,” alisema Kairuki.
Alisema hali ya miundombinu katika Shule hiyo ni mbaya na inabidi kurekebishwa haraka kutokana na baadhi ya madarasa kujengwa chini ya kiwango kutokana na kuta zake kuwa na nyufa miaka michache baada ya kukamilika kwa ujenzi.
Kaimu Mkurugenzi huyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya mifugo na uvuvi alisema hajui lolote kuhusu mchanganuo wa fedha iliyotolewa na Tamisemi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu, vyoo, madarasa na kuingiza umeme shuleni ingawa aliahidi kutekeleza agizo la Waziri Kairuki.
Mbunge wa Mbulu mjini, Zakaria Essau alisema ipo haja kwa Serikali kutoa waraka kuonyesha umuhimu wa kutunza majengo ya Serikali ambayo mengi yamekuwa yakiharibika muda mfupi baada ya kujengwa.
FUKUZA WOTE HAO ,WEKA NDANI NA KIFUNGO CHA MIAKA 30 KILA MMOJA
ReplyDelete