Zaidi ya nyumba 50 ikiwemo ya mkuu wa jeshi la polisi mstaafu katika manispaa ya moshi mkoani Kilimanjaro zipo hatarini kubomolewa wakati wowote baada ya kujengwa kinyume cha sheria ya mipango miji na sheria ya hifadhi ya mazingira ambayo ni kando ya mto Karanga.
Mkuu wa wilaya ya Moshi Bw.Novatus Makunga amesema hayo baada ya kukagua baadhi ya nyumba akiwa na kamati ya ulinzi na usalama na kujiridhisha juu ya ujenzi wa nyumba hizo kinyume cha sheria..
Bw.Makunga ambaye ameipa siku saba manispaa hiyo kutoa taarifa rasmi juu ya ujenzi holela amesema,serikali inafanya uchunguzi wa kuwabaini baadhi ya maafisa ardhi wa manispaa hiyo waliotoa vibali vya ujenzi wa nyumba hizo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo Bw.Danford Kamenya amesema, kamati hiyo pia imeyatembelea baadhi ya maeneo ambayo wafanyabiashara ndogondogo wamepanga bidhaa zao chini na kuangalia namna ya kuwatafuia maeneo mengine ya biashara.