Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), imeiandikia barua CUF, kuitaka kuwasilisha majina ya mawakala watakaosimamia uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika visiwani hapa Machi 20, mwaka huu.
Hata hivyo, CUF wameendelea na msimamo wao wa kutotambua uchaguzi huo na kuitaka ZEC iache kutapatapa, wakati walishaijibu kuwa hawatashiriki uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa makatibu wa CUF wa wilaya 10 za Zanzibar, Hamad Masoud Hamad ambaye ndiye aliyeandikiwa barua hiyo na ZEC, alisema wanashindwa kuielewa tume hiyo kwa kitendo cha chao cha kukitaka chama hicho na vyama vingine vishiriki uchaguzi huo kwa madai kuwa ni batili.
“Tunashindwa kuwaelewa ZEC, hivi wanachokitaka kwetu sisi ni nini haswa, tuliwaambia na barua tuliwaandikia kuwa hatutashiriki uchaguzi wa batili.
“Isitoshe juzi Maalim Seif (Seif Shariff Hamad) alisisitiza kuwa hakuna mgombea wa CUF atakayegombea akiwamo yeye na kuitaka ZEC iondoe jina lake,” alisema Hamad .
Katibu wa CUF Wilaya ya Unguja Mjini, Fadhili Sijaamini ambaye pia ni mwenyekiti wa makatibu wa wilaya wa chama hicho Zanzibar alithibitisha kupokea barua hizo Alhamisi ya wiki iliyopita kutoka kwa ofisa wa ZEC, ikimtaka apeleke orodha ya majina ya mawakala watakaosimamia uchaguzi huo, kisha nyingine asambaze kwa wenzake.
“Tunawashangaa sana ZEC ukweli upo wazi hawaeleweki na wamefikia pabaya na wanatapatapa,” alisema Sijaamini.
Aliongeza kuwa, yeye na makatibu wenzake wameshaiandikia barua ya kuijibu ZEC, kuwakumbusha msimamo wao kuwa hawashiriki kwa sababu hawautambui uchaguzi huo wa marudio.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa ZEC, Idrissa Hajji Jecha kuthibitisha taarifa hizo alidai kuwa yeye siyo msemaji wa tume hiyo na kumuelekeza mwandishi wa habari ampigie ofisa mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Muha.
Alipopigiwa Muha alikiri kupeleka barua hizo kwa kiongozi huyo za kuwataka CUF kupeleka orodha ya majina ya mawakala watakaosimamia uchaguzi huo.
Maskani CUF, CCM zachomwa
Hali ya hofu inazidi kutanda kila kukicha visiwani Zanzibar miongoni mwa wananchi kutokana na matukio ya uchomaji moto.
Hali hiyo inakuja huku zikiwa zimebaki siku chache kufanyika uchaguzi huo.
Wakati juzi maskani ya Kisonge inayomilikiwa na CCM ikiwa imelipuliwa kwa bomu la kienyeji, jana matawi ya CUF, zaidi ya matano yamelipuliwa kisiwani Pemba.
Maeneo yaliyochomwa moto ni pamoja na tawi la Mkanyageni lililopo Mkoani, Kiwapwa (Ziwani), Kiuyu Miningwini (Kojani), Ofisi ya jimbo la Wingwi na baraza la Konowe la Micheweni).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kaskazini Pemba, Shehani Mohammed Shehani, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kusisitiza kuwa wanaendelea na uchunguzi.
“Mimi sikuwepo katika hayo maeneo kwa sababu nilikuwa nimesafiri, lakini bado tunaendelea kuchunguza matukio hayo, huenda ikawa ni mbinu ya watu kutishwa ili wasijitokeze kwenye uchaguzi,” alisema kamanda huyo.
Akizungumza matukio hayo ya kuchomewa maskani zao Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema yametokea katika maeneo tofauti na kwamba wameripoti polisi.
“Kwa sisi hatuna la kufanya zaidi ya kwenda kuripoti polisi na kuwapa taarifa juu ya kuchomewa matawi yetu, na hilo tumelifanya asubuhi na mapema,” alisema Mazrui.
Mazuri alisema walitoa taarifa kwamba CUF imechoka kufanyiwa vitendo hivyo na kuwataka polisi wafanye kazi kwa maadili yao na siyo kufuata wanasiasa.
Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu Wilaya ya Micheweni, Kombo Mwinyi Shehe alisema matawi hayo ya yamechomwa moto usiku wa manane na kuteketea vibaya.
Shehe alisema ofisi ya jimbo ya Wingwi na baraza la CUF la Kinowe zilizopo Mkoa wa Kaskazini Pemba zimeteketezwa.
“Tulipokwenda tumeona moto mkubwa na kama unavyojua kumeezekwa makuti, na makuti yote yameshika moto kwa hivyo hata watu walipofika wameshindwa kufanya lolote kwa kuwa yalishateketeza jengo zima,” alisema Shehe.
Mbunge wa Wingwi, Kombo Juma Hamad alisema alipata taarifa katika jimbo lake kumetokea uchomaji moto huo na kuwasiliana na wenzake.
ZEC Yaibana Mbavu CUF Uchaguzi wa Marudio..Yaitaka Kuwakilisha Majina ya Mawakala Watakao Simamia Uchaguzi
0
March 07, 2016
Tags