ACT-Wazalendo Waishambulia CHADEMA

CHAMA cha ACT-Wazalendo Wilaya ya Shinyanga Mjini kimetamba kuwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ndicho kitakuwa mpinzani mkubwa wa CCM badala ya Chadema.

Katibu wa ACT-Wazalendo, Wilaya ya Shinyanga, Melkyoli Sebastian alisema hayo baada ya kumuingiza kwenye chama hicho, kada wa Chadema, Ibrahimu Mbogoma.

Mbogoma alikuwa mwenyekiti wa baraza la wazee kata ya Masekelo manispaa ya Shinyanga.

Sebastian alisema chama chao kimeanza kuaminiwa na wananchi kutokana na sera zake za kiujamaa ambazo zimelenga kumkomboa mwananchi wa hali ya chini bila ya kubagua dini, kabila wala rangi.

Alisema kutokana na sera hizo, ndiyo maana wanachama wa Chadema wameanza kujiunga na chama chao baada ya kusoma alama za nyakati.

“Kujiunga kwa kada huyo aliyekuwa Chadema ni salamu tosha kuwa Chadema inaelekea kufa kiupinzani, nina imani wapo wanachama wengi wa vyama vya upinzani watakuja kujiunga na ACT Wazalendo.

"Sisi tunawakaribisha waje kwa wingi ili tukijenge chama kuelekea Ikulu 2020,” alisema Sebastian.

Akieleza sababu za kuhama Chadema, Mbogoma, alisema ameamua hivyo kutokana na kuchoshwa na migogoro ndani ya Chadema pamoja na kuongozwa na viongozi wasiojua majukumu yao.

Mbogoma alisema tangu alipojiunga na Chadema mwaka 2010 hajaona mafanikio yoyote licha ya kushika nyadhifa mbalimbali. Alisema amekuwa akikumbana na migogoro ya mara kwa mara. Alisema anaamini ACT-Wazalendo ndicho kitaipindua CCM.

Katibu wa Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini, George Kitalama alisema alikuwa hajapata taarifa rasmi za kiofisi za kuhama kwa mwanachama wake huyo.

Hata hivyo, alisema kila mtu ana haki ya kwenda kujiunga kwenye chama anachokitaka kwa mujibu wa Sheria za nchi.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hilo liko wazi kwamba ACT-wazalendo ndio chama kitakachokuja kuitoa CCM madarakani kama wataendelea na msimamo huu walionao sasa.Hata 2015 walichokosea ni kumsimamisha mwanamke na sisi wengine imani zetu zinakingana mwanamke kuwa juu.

    ReplyDelete
  2. Kwel nyie mmekuja kudhoofisha upinzani badala ya kupanga mipango ya kukitoa chama tawala madarakadi mnajisifu kukidhoofisha chama cha upinzani.....

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad