Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limeanza kufanyiwa kazi baada ya karandinga kuanza kuwasomba ombaomba waliojaa katika maeneo mengi jijini hapa.
Makonda alitangaza kuanza kuwaondoa ombaomba hao juzi, huku akipiga marufuku wananchi kuwapa pesa kwa kuwa ndicho chanzo cha kuwapo kwao jijini hapa.
Zoezi hilo la kuwaondoa watu hao lilianza juzi usiku katika maeneo ya Mnazi Mmoja, Samora na Kariakoo.
Jana maeneo mbalimbali ambayo aghalabu ombaomba hupenda kukaa yalikuwa tupu.
Maeneo hayo ikiwamo barabara ya Morocco, Magomeni Usalama, Fire na Baridi hayakuwa na watu wa kundi hilo.
Mmoja wa ombaomba aliyekuwa na watoto wawili alipomuona mwandishi wa habari hizi katika maeneo ya Fire, alitimua mbio na kujificha pembeni mwa barabara, huku akisema: “Tumetoka Dodoma, hatutaki kurudi.”
Kadhalika, operesheni hiyo licha ya timuatimua kuwakumba ombaomba, wapigadebe nao wameunganishwa katika kundi hilo kwa kuanza kuondolewa kwenye vituo vya mabasi.
Baadhi ya wapigadebe hao wamedai ni vigumu kwa Makonda kuwaondoa kwa kuwa wanachofanya ni kwa manufaa ya maisha yao na hawana pa kwenda.
Agizo la kutaka ombaomba wakamatwe na kuondokana na vitendo hivyo liliwahi kutolewa pia na waliowahi kuwa wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba, Abbas Kandoro na Said Mecky Sadiki.