Akizungumza na MwanaHALISI Online leo Abdallah Posi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu) amesema, siyo jambo sahihi kwa walemavu hao kuishi kwa kutegemea kuomba na kwamba, kitendo hicho kinakandamiza fikra zao za kutafuta njia mbadala ya kujikwamua kiuchumi.
“Siyo sahihi kwa walemavu wanavyoishi kwa kutegemea kuombaomba kutokana na kwamba, kitendo hicho kinadumaza fikra zao na kusababisha hata wale wenye uwezo wa kujinyanyua kiuchumi kushindwa kufanya hivyo,” amesema Posi.
Amesema, kati ya walemavu hao wapo baadhi yao wana ndugu na jamaa ambao wanauwezo wa kuwasaidia na kwamba, siyo wote ambao hawana mahala pa kuishi.
“Hao walemavu wana ndugu na jamaa zao, serikali itahakikisha inawawajibisha ili wawajibike kutunza ndugu zao ambao ni walemavu ili waache kuishi maisha ya kuomba kwa kuwa, hawana sababu ya kufanya hivyo,” amesema.
Anaeleza kuwa, serikali inatafuta njia za kuwawezesha kiuchumi ili waondokane na dhana ya kuishi kwa kuomba na kwamba, kwa wale wenye uwezo wa kufanya kazi watatafutiwa vyanzo vya ajira kama walivyofanya baadhi ya walemavu wanaoendesha bajaji katika Jiji la Dar es Salaam.
Pembezoni mwa barabara kuu zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam wakati wa mchana, huzagaa ombaomba ambao kati yao ni walemavu.