Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake kesho watapata fursa ya kulitumia kwa mara ya kwanza Daraja la Kigamboni litakalofunguliwa rasmi na Rais John Magufuli, Jumanne wiki ijayo.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Joseph Nyamhanga ilieleza jana kuwa pia, Rais Magufuli kesho atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya Tazara jijini hapa.
Akizungumzia ujenzi wa daraja la Kigamboni, Meneja mradi wa Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group wanaotekeleza mradi huo kwa ushirikiano na Kampuni ya China Railway Major Bridge Group, Zhang Bangxu, alisema kesho watawaruhusu wakazi wa jiji na magari kupita bila kutozwa fedha katika daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu Dola 135 milioni za Marekani (takribani Sh283.5 bilioni).