Championi Jumatano linafahamu kwamba, Kessy anawaniwa na Yanga na Azam FC hivi sasa kwani amebakisha mwezi mmoja tu katika mkataba wake na Simba, hivyo yupo kuzungumza na klabu yoyote.
Hata hivyo, Kessy ni kama yupo huru kabisa kwani Simba imemsimamisha kucheza mechi tano ambazo zitachezwa ndani ya mwezi mmoja kwa kosa la kumchezea rafu Edward Christopher wa Toto Africans na kupewa kadi nyekundu.
Inafahamika kwamba, Yanga ndiyo ipo kwenye nafasi kubwa ya kumsajili Kessy kwani inataka acheze beki ya kulia huku beki wake Juma Abdul akipandishwa juu kucheza kama winga.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kessy alisema jezi namba 25 ndiyo yenye bahati kwake na siri kubwa kwake, hivyo timu itakayofikia makubaliano mazuri ya kumsainisha, basi ihakikishe inampatia jezi hiyo.
Kessy alisema, moja ya siri ya namba hiyo 25, ni tarehe yake ya kuzaliwa, hivyo ameichagua jezi hiyo kwa ajili ya kuipa heshima kwenye msimu ujao wa ligi kuu.
Aliongeza kuwa, awali wakati anatua kuichezea Simba alipanga kuivaa jezi hiyo, lakini ikashindikana kutokana na kukuta ikivaliwa na mshambuliaji wa timu hiyo, Ibrahim Ajib.
“Kutokana na mikosi niliyoipata nikiwa naichezea Simba nimeona niachane na namba nne niliyokuwa ninaivaa ili huko ninapokwenda kupya ili mikosi nisiwe nayo, nimepanga kuvaa jezi namba 25.
“Nipo kwenye mazungumzo na timu nyingi, na kinachosubiriwa ni kufikia makubaliano mazuri katika mahitaji yangu ambayo kama tukikubaliana nitakwenda kuivaa hiyo jezi yangu mpya.
Jezi hiyo namba 25 hivi sasa haivaliwi na mchezaji yeyote katika kikosi cha Yanga na mara ya mwisho ilikuwa inavaliwa na Emmanuel Okwi aliyetimkia Simba na baadaye Sønderjyske ya Denmark.
Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh aliliambia Championi Jumatano kuwa, jezi namba 25 haina mvaaji Yanga lakini hakuwa tayari kuzungumzia usajili wa Kessy.