Kamanda Mstaafu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova (pichani) ameibuka kufuatia ‘kubumburuka’ kwa sakata linalomhusu mfanyabiashara Said Lugumi, anayemiliki kampuni ya Lugumi Enterprises inayodaiwa kuingia mkataba tata na Jeshi la Polisi Tanzania.
Mkataba kati ya Lugumi Enterprises na jeshi hilo ulisainiwa mwaka 2011, ulihusu kufungwa kwa vifaa vya kuchukulia alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya shilingi bilioni 37. Lakini hadi sasa, vifaa hivyo vimefungwa katika vituo 14, vyote vikidaiwa kuwa ni vya Dar es Salaam lakini bila kujulikana sehemu.
Kova, ndiye aliyekuwa Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam wakati vifaa hivyo vikifungwa katika vituo 11 vya Polisi huku ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi ikiwa chini ya Said Mwema. Kampuni hiyo inadaiwa kulipwa karibu asilimia 99 ya fedha zote za makubaliano.
Akizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki iliyopita, Kova ambaye alidai yupo kijijini kwao akijishughulisha na kilimo, alisema hajui lolote kuhusu Lugumi, kwa sababu kule aliko hakuna magazeti wala vyombo vingine vya habari zaidi ya mitandao.
“Mimi nilikuwa nashughulika na wahalifu na Lugumi hakuwa mhalifu, siwezi kumzungumzia lolote kwa sababu mimi nimeshastaafu. Huku nilipo sipati taarifa zozote za kiofisi, nimekuwa kama samaki nje ya maji, sina nguvu zozote,” alisema kamanda huyo.
Aliongeza: “Lakini Lugumi namfahamu ila si kwa hilo sakata la vifaa vya kuchukulia alama za vidole ndugu yangu.”
Sakata la Kampuni ya Lugumi Enterprises liliibuliwa kwa mara ya kwanza na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Makamu Mwenyekiti, Aeshi Hilary, April 6, mwaka huu, baada ya kubaini utata wa utekelezaji wake na kuagiza kupelekwa kwao ili kujua masharti yaliyomo.
GPL