Kamati ya Bunge ya Masuala Ukimwi na Dawa za Kulevya, imeitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kueleza hatua ambazo imekwishazichukua baada ya Rais mstaafu wa Jakaya Kikwete, kutangaza hadharani kuwa ana orodha ya majina ya wafanyabiashara wakubwa wa mihadarati.
Ilionya kuwa kuchelewa kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao, kumeongeza idadi ya watumia dawa hizo magerezani huku Watanzania zaidi ya 160 wakifungwa nchini China baada ya kukamatwa wakisafirisha dawa hizo.
Mjumbe wa kamati hiyo, Grace Tendega, (Viti Maalum Chadema), alimtaka Waziri wa wizara hiyo, Charles Kitwanga, kutoa maelezo ya hatua za kisheria zilizokwishachukuliwa baada ya JK kueleza taarifa hizo.
“Rais Kikwete alitangaza hadharani kwamba tayari amekabidhiwa orodha ya majina ya wauza unga, Jeshi la Polisi limechukua hatua gani kushughulikia suala hili,? Vijana wetu wanaotumia mihadarati wanaongezeka na wengi wanaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU),” alisema Tendega.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo Elibariki Kingu , Singida Magharibi (CCM), alihoji namna Jeshi la Polisi linavyoimarisha ulinzi katika mipaka, kudhibiti bandari bubu hususan iliyopo Mbweni jijini Dar es Salaam, kwani inaongoza kwa kupitisha magendo na dawa hizo.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, John Kadutu, alisema matumizi ya dawa za kulevya yameongezeka migodini akihoji uhakika na usalama wa watoa taarifa kuhusu dawa hizo, kwani wengi wao wamekuwa hawafichiwi siri.
Akijibu hoja hizo, Kitwanga alisema hajawahi kuiona orodha ya majina ya wauza dawa za kulevya, ambayo alikabidhiwa Rais mstaafu Kikwete na badala yake wizara imeendelea kufuatilia mfumo na mtandao wa mihadarati kwa kushirikiana na idara nyingina za serikali ikwamo ya Uhamiaji na Jeshi la Magereza.
“Serikali ya awamu ya tano ina dhamira ya kupambana na dawa hizo ndiyo maana kwa Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali tayari amegundua sampuli 294 za dawa za kulevya kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, wakati mwaka jana mzima zilipatikana sampli 282 pekee,” alisema Kitwanga.
Naye Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja , alisema kuwa, matumizi ya mihadarati kwa wafungwa yameongezeka magerezani, kutokana na askari wasio waaminifu, watu wanowatembelea kuwapelekea dawa hizo kwa njia mbalimbali.
“Tunatumia teknolojia ya kizamani kukagua wafungwa waliotoka nje ya gereza kutoka kwenye shughuli nje, wanakaguliwa lakini wanazificha dawa katika maeneo nyeti ya mwili ambayo haki za binadamu zinakataza kuwashika, pia ndugu zao wanawekea katika maji, mkate au sabuni na kusababisha kukithiri kwa dawa gerezani,” alisema Minja.
Aliwaambia wajumbe kuwa kucheleweshwa kwa kesi kunawafanya watuhumiwa wa dawa za kulevya kukaa kwa muda mrefu gerezani, jambo linalo hatarisha usalama wa magereza na nchi kwani watu hao wanamtandao mkubwa kimataifa.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, alisema mchakato mrefu wa kuthibitisha wanaotuhumiwa kuuza dawa za kulevya, unatokana na upepelezi kuchukua muda mrefu kwani jeshi hilo linashirikiana na idara za serikali akiwamo Mkemia Mkuu , kisha kesi kupelekwa kwa mwendesha Mashtaka (DPP) hatimaye mahakamani.