Polisi mkoani Mwanza, ndugu, jamaa na marafiki, juzi, walilazimika kufukua kaburi na kutoa mwili wa Gelinde Masumbuko baada ya kuzikwa na ndugu wa marehemu Said Mussa na kukaa kaburini kwa siku mbili.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Mwanza wa Sekou-Toure, kuukabidhi mwili wa Masumbuko kwa ndugu wa Mussa.
Baada ya kukabidhiwa mwili huo, ndugu wa Mussa waliendelea na taratibu na kuuzika katika makaburi ya Nyashana wilayani Ilemela, kabla ya ndugu wa Masumbuko kubaini kuwa mwili wa ndugu yao uliokuwa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hauonekani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema walilazimika kuingilia kati suala hilo baada ya ndugu wa Masumbuko kuripoti tukio la mwili wa ndugu yao kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Baada ya uchunguzi kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali tulibaini yalifanyaka makosa kwa mwili huo kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu Mussa ambao tayari walishauzika,” alisema.
Uchunguzi huo ulibaini mwili wa Mussa ulikuwa bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
“Ilibidi taratibu za kisheria zichukuliwe na mwili wa marehemu Masumbuko kufukuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu zake, huku ndugu wa Mussa nao wakichukua mwili wa ndugu yao kwa mazishi mapya,” alisema Kamugisha.
Mkanganyiko huo ulitokea baada ya ndugu wa Masumbuko kutoka Sengerema kufuata mwili katika hospitali hiyo na kuukosa, hali iliyowalazimu kufuatilia ili kujua alikozikwa na taratibu za kuufukua zifuatwe.
Ndugu wa Masumbuko, Finias Elias, alisema walitarajiwa kumzika jana nyumbani kwao wilayani Sengerema.
Ndugu wa marehemu Mussa, Said Mussa alisema waliotumwa kuuchukua mwili wa marehemu walishindwa kumtambua kutokana na kuvimba uso.
Du! inanikumbusha ile inshu ya hospitali ya Bombo Tanga...
ReplyDelete