WANANCHI wamemkataa mwenyekiti wa kitongoji cha Mwanogi kijiji cha Bulima, Kata ya Nyashimo wilayani hapa katika Mkoa wa Simiyu, wakimtuhumu kuweka majina hewa katika mradi wa kuokoa kaya masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Mwenyekiti huyo wa kitongoji, Ester Ng’ombe anatuhumiwa pia kufanya kazi kwa ubaguzi wa vyama vya siasa.
Akizungumza katika kikao, mwenyekiti wa kamati ya mipango na fedha ya kijiji cha Bulima, Zablon Ntinika alisema wamefikia uamuzi wa kumsimamisha kazi mwenyekiti huyo baada ya uchunguzi walioufanya kubaini majina matano ambayo ni hewa yakipatiwa fedha.
Alisema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa mwenyekiti huyo katika utendaji wake wa kazi katika kitongoji hicho lakini wamebaini mengi. Mwenyekiti huyo anayetuhumiwa, alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema kuwa yeye hayatambui bali ni siasa za chuki dhidi yake.
Ng’ombe alisema chanzo si majina feki bali ni siasa zinazochochewa na wanasiasa wa kata hiyo ambao wanataka kuichafua sifa yake ili aweze kuondolewa na wananchi waliomchagua.