Mfayakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini aliyetuhumiwa na Rais John Magufuli mwezi uliopita kujilipa mishahara 17 ya watumishi hewa, hayupo kwenye ajira ya TRA kwa siku nyingi zilizopita, imefahamika.
Habari kutoka ndani ya Mamlaka hiyo zimesema kuwa mfanyakazi huyo alikuwa ni wa Idara ya Uhasibu ya TRA lakini alishafukuzwa kazi siku nyingi zilizopita.
Chanzo cha kuaminika kutoka Makao Makuu ya TRA kimeiambia Nipashe kuwa mfanyakazi huyo alifukuzwa kazi baada ya kubainika kujilipa mishahara hiyo katika akaunti yake.
Chanzo chetu cha habari ambacho hakikupenda kutajwa jina kwa sababu si msemaji wa mamlaka, kilisema mfanyakazi huyo baada ya kuhojiwa alikiri kujilipa mishahara hiyo.
“Huyu mfanyakazi alikuwa Idara ya Uhasibu… ni kweli alijilipa mishahara hiyo na baada ya kuhojiwa alikiri ndipo tukamfukuza kazi na kumpeleka mahakamani,” chanzo hicho kilieleza.
Rais Magufuli alimfichua mfanyakazi huyo hivi karibuni akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita, alipokuwa alihutubia kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais Oktoba 25, mwaka jana.