Mbunge wa jimbo la Nyamagama,jijini Mwanza pichani akifurahia mara baada ya kutangazwa mshindi wa jimbo hilo na Mahakama kuu ya jijini Mwanza dhidi ya aliyekuwa Mgombea Ubunge wa jimbo hilo kupitia chama cha CHADEMA,Mh.Ezekiel Wenje.
****EZEKIEL Wenje, mbunge wa zamani wa Jimbo la Nyamagana, Mwanza ameshindwa kwenye kesi aliyoifungua katika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga dhidi ya Stanslaus Mabula.
Mahakama hiyo leo imempa ushindi Mabula (CCM) baada ya kujiridhisha kuwa, upande wa madai hauna ushahidi unaokidhi, kuithibitishia mahakama.
Wenje alifungua kesi hiyo akipinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo mwaka jana yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kumpa ushindi Mabula.
Katika kesi hiyo namba tatu ya mwaka 2015, ambayo ilionekana kugusa hisia za wakazi wa Nyamagana imehudhuriwa na idadi kubwa ya wafuasi wa upinzani na CCM.
Akitupilia mbali shauri hilo leo Kakusulo Sambo, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga amesema kuwa, amefikia hatua hiyo baada ya upande wa mpeleka maombi kuiomba mahakama kuifunga kesi hiyo.
Amesema upande wa mpeleka maombi, ulidai kwamba kutokana na ombi lao la kupokelewa kwa fomu namba 21B kukataliwa kortini hapo, ulidai hakuna umuhimu wa kuendelea kwa kesi hiyo.
Jaji Sambo amesema, upande wa mpeleka maombi, licha ya kupewa muda wa siku 10 kupeleka fomu namba 21B lakini hawakufanya hivyo.
Amesema, pamoja na kuchelewa kupeleka fomu hiyo pia walipopewa muda wa kujieleza katika ombi lao la kuiomba mahakama kupokea fomu hizo, hawakueleza sababu za msingi.
Hata hivyo amesema baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo kortini, mahakama ilikaa na kutafakari kwa kina juu ya ombi hilo ambapo imeamua kutupilia mbali kesi hiyo.
“Mleta maombi aliomba kufunga kesi mahakamani na mahakama sasa imepitia ombi lao, hivyo na kuona kesi hii haina msingi wowote ule na tunakubaliana nao,” amesema Jaji Sambo.
Hata hivyo wakati shauri hilo likitupiliwa mbali kortini hapo, Wenje pamoja na wakili wake, Deya Outa hakuwepo mahakamani hapo bila taarifa yoyote.