Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyoko The Hague nchini Uholanzi imefuta kesi dhidi ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto na mwandishi wa habari Joshua Arap Sang waliokuwa wakituhumiwa kuhusika katika vurugu na mauaji ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Majaji wa ICC wameeleza kuwa wameamua kuiondoa kesi hiyo baada ya kuwepo kwa mkanganyiko katika ushahidi uliofikishwa mahakamani.
Baadhi ya mashahidi walianza kubadili ushahidi wao huku wengine wakijiondoa kwa madai kuwa walishinikizwa au kushawishiwa kutoa ushahidi huo.
Katika uamuzi wao, majaji hao wameeleza kuwa kuondolewa kwa kesi hiyo hakuwazuii wawili hao kushtakiwa tena kwenye mahakama hiyo au mahakama nyingine ya kimataifa na kitaifa.
Uamuzi huo wa ICC umepokelewa kwa hisia tofauti nchini humo. Wapo walioufurahia na kueleza kuwa kesi hiyo ilijaa mihemko ya kisiasa zaidi na kwamba kwa kuachiwa huru Ruto atakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kuwatumikia wananchi wake kwa umakini zaidi.
Lakini wapo wanaolalamikia uamuzi huo wakiwaangazia hasa wahanga wa machafuko hayo yaliyopelekea mauaji ya zaidi ya watu 1000 na kuwakosesha makazi maelfu ya raia.
Waathirika wa tukio hilo wanaonekana kuwa katika hali ya sintofahamu zaidi kwani uamuzi wa mahakama hiyo haukufikia hatua ya kuweza kubainisha iwapo Ruto na Sang walikuwa na hatia.