Akizungumza na Umoja wa Vijana Waendesha Bodaboda wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Viwanja vya Leaders Club jijini humo leo, Makonda amesema wapinzani wataishia kuchongwa, na kwamba, mamlaka ya jiji hilo yapo mikononi mwake.
Kauli yake inafanana na iliyotolewa na Said Meck Sadick, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati akikabidhi ofisi hiyo siku chache zilizopita.
Makonda ametoa kauli hiyo siku tatu baada ya Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kutangazia umma kwamba licha ya uanachama wake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), atafanya kazi bila kujali itikadi za vyama vya siasa.
“Mamlaka ya uamuzi ya utendaji kazi Mkoa wa Dar es Salaam yako mikononi mwangu. Wengine wataishia kusema wee,watapiga domo wee, lakini mwenye mamlaka ya mwisho katika uamuzi ni mimi,” alitamba Makonda.
Mimi ndiyo Rais wa Dar es Salaam.Ninayo mamlaka ya kukataa chochote wanachopanga hawa wapinzani; Ni lazima mipango yao yote wailete kwangu na nitaamua kwa maslahi ya wananchi na si vinginevyo; Makonda alizidi kutamba kwa kejeli.
Kauli hiyo ya Makonda ni muendelezo wa mikogo yake dhidi ya UKAWA ambao tayari wameonesha dhamira ya kuachana na migogoro ya kisiasa ili kuhudumia wananchi.
“Msiwe kama baadhi ya viongozi wa waendesha bodaboda wanaofuata wanasiasa na kuwatajia idadi ya wanachama wanaowamiliki ili wapate hela na kutumikishwa kisiasa ili wafanye fujo halafu waanze kusema, serikali haifanyi kitu, haithamini wananchi wake na mambo mengine ya kisiasa,” Makonda aliwaambia bodaboda hao.
Aidha, ametoa maagizo kwa Simon Sirro, Kamanda Mkuu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akimtaka ashughulikie matatizo ya waendesha bodaboda.
“Ndani ya siku 90 kabla ya kupatikana kwa Kamati ya Kudumu ya Umoja wa Waendesha Bodaboda, nakuagiza Sirro ukawaambie polisi wako waache kuingilia matatizo ya waendesha bodaboda, bali polisi wawe washauri wa shughuli zinazofanywa nao,” amesema.
Makonda ametaja takwimu za ajali na vifo vilivyosababishwa na bodaboda katika Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2015. Takwimu hiyo inaonesha kutokea kwa ajali zaidi ya 1000 na vifo 100.
“Katika Wilaya ya Ilala, ajali zilizotokea ni 486, vifo 34, Temeke 542, vifo 31 na Kinondoni ajali 170 na vifo 36,” amesema.Daud Laurian, Katibu wa Kamati iliyomaliza muda wake, wakati akisoma risala, amemtaka Makonda kushughulikia baadhi ya wajumbe wa Saccos ya umoja huo (DABOSA) kwa kosa la kufanya ubadhilifu wa fedha zao kiasi cha Sh 50 milioni.
“Tunakuomba Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, uwatumbue baadhi ya viongozi wa Saccos yetu ambao wamefuja fedha zetu shilingi milioni 50 kwa manufaa yao binafsi,” amesema Laurian.
Chanzo: MwanaHalisi Online