Sauti za viongozi wawili wa juu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesikika wakijadili namna ambavyo wanaweza kuisaidia timu moja kupata ushindi.
Viongozi hao, wanaeleza wanavyotaka kitita cha fedha, Sh milioni 10, walipwe viongozi wengine, Sh milioni 10, nyingine kwa ajili ya moja ya kamati za TFF na baada ya hapo Sh milioni 5, ambayo atapewa ofisa mwingine wa shirikisho hilo ili aende kuzungumza na wakubwa wa Idara ya Uhamiaji ambako inatakiwa kumkandamiza mchezaji wa timu fulani ili nyingine ipate ushindi.
Siku moja tu baada ya sauti hizo kusikika, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Martin Chacha akatangaza kuachia ngazi, huku akisema ni kutokana na kubanwa na matatizo ya kifamilia.
Gazeti hili likafanya mahojiano na Juma Matandika, kutaka kujua vipi alishiriki kwenye kikao hicho, akasisitiza anaamini sauti zao zimeigizwa kwa kuwa na watu wengi wana uwezo wa kuigiza huku akimtaka mwandishi kama naye anataka sauti yake iigizwe, basi aende ili ampeleke.
Tuliacha hilo, tuamini kabisa Rais wa TFF, Jamal Malinzi, hawezi kuhusika na kitu kama hiki na waliokwenda kutenda jambo hilo walifanya bila ya kumueleza kwamba wana ujanja wanaofanya. Lakini najiuliza, yeye atalikwepa vipi?
Wote tunajua suala hili linahusiana na rushwa, adui wa haki, adui wa mpira wa Tanzania na adui wa nchi yetu, lakini naona kuna ujanja unafanyika kuona hili linaonekana limetengenezwa.
Najua lazima Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) haitaliacha lipite hivihivi na hasa ukizingatia serikali ya sasa ni ile inayotaka mambo yaende kwa haki na uamuzi wake ni haraka, si kama ilivyokuwa katika awamu nyingine zilizopita za uongozi.
Nimeanza kuona harufu ya njama zinazoanza kutengenezwa kutaka kulifanya jambo hili lionekane ni bahati mbaya au halikuwahi kabisa kutokea.
Kuna mipango inatengenezwa ili ionekane kwamba waliosikika sauti zao zimetengenezwa na kuna lengo la kuwadhalilisha. Lakini naona hata TFF yenyewe inataka kuingia mkenge kutaka kuanza kuzuia vyombo vya habari kuliripoti jambo hili, niwahakikishie mtafeli.
Huenda ni njia ya kutaka kutulazimisha kwa ulaini kuamini maelezo ya Matandika? Kwamba sauti zao zimetengenezwa? Jamani, uoneeni huruma mpira wa Tanzania nanyi muwe na aibu kiungwana!
Niliona taarifa yao waliyoitoa TFF siku moja baada ya sakata hilo, wakisisitiza kwamba wanaonya viongozi wa juu wa shirikisho hilo kuhusishwa na sakata hilo.
Kwangu ninaona ni kuingilia uhuru wa vyombo vya habari, kwangu naona ni kulazimisha kuwafumba midomo waandishi wa habari kwa lengo la kufunika maovu kwa nguvu, jambo ambalo haliwezi kuvumilika wala halitakuwa na nafasi kwangu.
Sauti zinazosikika, zinajulikana ni za kina nani. Wanaozungumza ndiyo viongozi wa ngazi za juu. Sasa unashindwa vipi kuwahusisha na viongozi wa ngazi za juu?
Viongozi wa ngazi za juu wanakwenda vipi katika hili na wengineo wametajwa ndani yake. Hata kama waliotaja ingekuwa hatuwajui, basi isingekuwa rahisi kuruka maneno waliyosema hasa yale waliotaja viongozi wa juu wa TFF.
Ninachomshauri Rais wa TFF, Jamal Malinzi ni kujiandaa. Kuwa tayari, kukaa mguu sawa kama itathibitika wahusika walichofanya kupitia vyombo vya dola, basi yeye ajivue madaraka kwa kuwa atakuwa amechafuliwa na aliowaamini.
Tulilalama kuhusu tuhuma za rushwa kwenye soka, sasa tuhuma ziko ndani ya shirikisho, waliopewa dhamana ya kuuendesha mpira, nini maana yao wao kuwepo? Kwani waliojiuzulu wote ni wale waliopatikana na hatia tu, kuhofiwa ni kuondolewa kwenye uadilifu tena kwa njia kama hiyo ya sauti.
Hii ndiyo kashfa kubwa zaidi kutokea katika shirikisho hilo tokea kuanzishwa kwake. Nakumbuka kiongozi wa Chama cha Soka Tanzania (Fat), alifungwa jela. Lakini TFF haikuwa imewahi kuchafuka kwa kiwango hiki.
Tena inachafuka kipindi ikiwa imetoka kutoa adhabu kupitia moja ya kamati zake ambayo iliwafungia wachezaji, waamuzi na viongozi kwa madai ya kupanga matokeo. Haki iko wapi sasa?
Badala ya kupambana kuizima, kwa kutaka kuwaziba watu midomo kwa nguvu. Huu ni wakati wenu wa kutafakari na kutengeneza mwisho wa kuongoza kwa matamanio ya maendeleo ya nafsi zenu na kuwaacha wenye nafasi ya kuongoza kwa lengo la kuleta maendeleo kwenye mpira wa Tanzania. Leo nimeanza, kesho nitarudi tena, nina mengi ya kusema.
Imeandikwa na Saleh Ally
Source: salehjembe.blogspot
Malinzi Hana Nafasi ya Kulikwepa hili la Upangaji Matokeo, Lazima Ajiuzulu – Mchambuzi
2
April 09, 2016
Tags
Hii kweli kali, mchezaji kaenda kunya anafungiwa miaka 10, tena ni golikipa wa timu iloshinda duh! Hebu oneni aibu basi, kuweni hata na huruma kwa watoto wa'wenzenu...JAMANI TFF HII IMEOZA INANUKA UVUNDO
ReplyDeleteHaya ndio yale yale ya Mwadui, ndio yaleyale ya Ruvu Shooting, viongozi wa TFF Shinyanga wanapenda mteremko...HAKI NI LAZIMA ITENDEKE KWA HARAKA
ReplyDelete