Mr Blue analalamika kuwa Sugu ameupora wimbo wake ‘Freedom’ aliokuwa amemshirikisha kwa kutoa verse zake na kuufanyia video iliyotoka jana.
Lakini katika kila malalamiko, ni vyema kusikiliza pande zote zinazohusika kwenye jambo husika ili kuupata ukweli. MJ Records walioutayarisha wimbo huo wamezungumza kuelezea mambo yalikuwaje.
Producer mkuu wa studio hiyo, Marco Chali ameiambia Bongo5 kuwa beat ya wimbo huo ilitengenezwa na mdogo wake, Daxo Chali aliyetengeneza chorus yake na alimpa msanii wake Lizzy aliyeingiza. “Ngoma ilikuwa ipo tayari na ilikuwa inasubiria verse tu kadhaa halafu ilikuwa ni ngoma yake [Daxo]. Kwahiyo jamaa [Blue] akawa ameipenda tukampa akasema atamshirikisha Mr Two,” amesema Marco.
Walipoifanya, Blue aliiamua kuiachia kupitia Mkito peke yake kwa maana kwamba hakuiachia ngoma rasmi. Anasema baada ya muda Sugu alimpigia simu kumuomba kuwa afanye version nyingine ya wimbo huo na aifanyie kabisa na video.
Anadai alimuambia Sugu aongee na Daxo waliyekubali kuufanya tena hadi video ikafanyika huku yeye [Marco] akiwa hajui chochote kilichoendelea baada ya hapo. Na Marco anasema pia hakuhusika kwenye uingizaji wa sauti zote mbili zaidi ya kuzifanyia mixing peke yake.
Marco amesema anadhani wawili hao [Sugu na Blue] waliongea kuhusu hatua hiyo na kwamba wao kama studio hawakuwa na kipingamizi chochote kuhusu kurudiwa kwa wimbo huo kwasababu walitaka wimbo ufike mahali.
Hata hivyo Marco amedai kuwa wote wawili [Sugu na Blue] hawakulipia wimbo huo na kwamba MJ Records iliwapa kwasababu ya ‘love’ tu. Marco anasema anashangaa kuona Mr Blue sasa hivi anatoa malalamiko hayo. “Ni kwasababu mimi nilipenda tu kutoa studio bure kwanini usijitahidi ukapeleka hiyo nyimbo ikafika sehemu ikafahamika, at least pia akili za watu zilizotumika watu wazione. Na ndio hicho kitu naona ni kizuri, yeye kwa mfano angefanya hata video, sidhani kama Sugu angerudia huo wimbo,” ameongeza Marco.