Mbowe Ataja Sababu 3 Zilizomfanya Awaongoze Wabunge wa UKAWA Kususa na Kutoka Nje Ya Ukumbi wa Bunge

Kambi ya Upinzani bungeni jana imesusia kuwasilisha na kujadili hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, huku kiongozi wake, Freeman Mbowe akitoka nje ya ukumbi huo, akitaja kasoro tatu zilizosababisha wachukue uamuzi huo.

Staili ya kususia kujadili hotuba hiyo ya bajeti ni mpya kwa kambi hiyo ya upinzani baada ya kutumia njia ya kutoka nje ya ukumbi wakati wa vikao vya Bunge la Katiba na baadaye kutumia njia ya kupiga kelele kukwamisha shughuli za chombo hicho wakati wa Bunge la Kumi.

Jana, Mbowe aliwaambia waandishi nje ya ukumbi kuwa kasoro zilizofanya wachukue uamuzi huo ni kukiuka masuala ya kisheria katika utekelezaji wa bajeti, kutotangaza kwenye Gazeti la Serikali mabadiliko ya wizara na kutorushwa kwa vipindi vya Bunge kwenye televisheni.

Mbowe, ambaye alikuwa akitarajiwa kusoma bajeti ya upinzani kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu, aliibuka na hoja hizo tatu kabla ya kuamua kutoka nje.

“Bajeti inakuwapo kwa sababu ni hitaji la kisheria. Inapokuwa Serikali inataka kupitisha bajeti, lakini haiheshimu bajeti hakuna sababu ya wabunge kukaa hapa kujadiliana, kutoa povu, kupitisha vifungu vya Katiba, halafu yenyewe haitekelezi wajibu wake kisheria,” alisema Mbowe nje ya ukumbi wa Bunge.

Alisema Serikali imekuwa ikikiuka sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri inayomtaka Rais kutengeneza mwongozo wa muundo wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake, ikiwa ni pamoja na kutangaza katika gazeti la Serikali mabadiliko ya wizara zake.

Alisema “Tulichelewa kuunda (Baraza Kivuli la Mawaziri) kwa sababu tulikosa instrument (nyaraka rasmi). Tukalazimika kuunda hivyohivyo. Sasa tumefika kwenye (Bunge bado Serikali haijaundwa officially (rasmi), kisheria. Haijawa gazetted (haijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali),” alisema Mbowe.

“Mpaka leo Serikali hii inafanya kazi kwa kutumia instrument iliyosainiwa na Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete mwezi wa 12 mwaka 2010.

“Na wizara kuu kwa mujibu wa instrument ya mwaka 2010 ilikuwa ni Wizara ya Waziri Mkuu Tamisemi. Na Tamisemi ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo baada ya uchaguzi wa 2010, Tamisemi imerudishwa Ofisi ya Rais, haiku tena Ofisi ya Waziri Mkuu. Lakini haijawa gazetted.”

Alitaja hoja nyingine kuwa ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusiana na bajeti unaofanywa na Serikali pamoja na kuminya uhuru na madaraka ya mhimili wa Bunge kwa kuzuia matangazo ya wasusia Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.

“Hatutashiriki mjadala tunaendelea kutafakari hatua nyingine za kuchukua kama Serikali na Bunge hawatatafuta ufumbuzi wa masuala hayo matatu,” alisema Mbowe.

Mbowe aliingia ukumbini saa 9:56 alasiri akiongozana na mbunge wa Momba, David Silinde na alikwenda kusalimiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) George Masaju na Waziri wa Kilimo, Mwigulu Nchemba.

Mara baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge, Mbowe alieleza sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ambapo alidai kifungu cha 5(1) kinaweka masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu yake.

Alisema mpaka sasa Serikali inafanya kazi bila kuwa na mwongozo wa utendaji kwa wizara mbalimbali hivyo kazi nyingi za Serikali zinafanywa kwa kauli ya Rais.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali kwa kila wizara unaotumika ni uliochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 494 A la Desemba 17, 2010 ambao pia umetoa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kiongozi huyo alinukuu baadhi ya majukumu katika mwongozo huo kuwa ni kuratibu shughuli za Serikali, kiongozi wa Serikali ndani ya Bunge, kiungo kati ya Bunge na Serikali, shughuli za kisiasa na serikali na kuratibu sherehe na misaada mbalimbali.

“Kazi nyingine ni kusaidia urahisishaji wa mipango ya serikali katika kuhamishia makao makuu Dodoma, uwekezaji, uchumi, sekta binafsi na kusaidia maendeleo katika sekta za ndani,” alisema Mbowe.

Alisema Rais John Magufuli alifanya mabadiliko ya kuziunganisha wizara bila kubadili muongozo wa kisheria.

“Kitendo cha Serikali hii kuendesha kazi zake kwa mwongozo wa 2010 kina maana kwamba majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu bado ni yale yale ya mwaka 2010 kwa sababu gazeti hilo halijafutwa,” alisema.

Alifafanua kuwa jambo hilo ni uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusu bajeti unaofanywa na serikali na kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge limepewa mamlaka ya kujadili utekelezaji wa kila wizara na kuidhinisha bajeti ya Serikali.

Mbowe alisema ikiwa fedha zilizoidhinishwa na bunge hazikutosha kutekeleza majukumu, kifungu cha 41 (1) cha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kinaelekeza kuwa serikali itawasilisha bungeni maombi ya idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango.

Alituhumu kuwa kumekuwa na uvunjwaji wa kifungu hicho na kutolea mfano bajeti ya Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka wa 2015/16 ilikuwa Sh 883.8 bilioni ambazo kati ya hizo, fedha za ndani zilikuwa Sh191.6 bilioni.

 “Jambo la kushangaza ni kwamba hadi kufikia mwezi Machi 2016 Wizara ilikuwa imeshapokea kutoka hazina Sh607.4 bilioni ikiwa ni fedha za ndani, kitendo kinachoonyesha kuwa na ongezeko kubwa la fedha za ndani,” alisema.

Alitaja kuwa tangu kuidhinishwa kwa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, hakuna bajeti ya nyongeza iliyopelekwa bungeni na Serikali kwa ajili ya kupata idhini kutokana na matakwa ya Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 au sheria ya fedha ya 2015.

 “Kitendo cha Serikali kuamua kuhamisha kiasi cha fedha ya bajeti bila ya kupata idhini ya Bunge ni dharau kwa bunge lakini mbaya zaidi ni uvunjwaji wa Katiba na sheria.” alisema.

 Nje ya ukumbi wa Bunge alisema:”Ukiwauliza wanapata wapi hizi fedha, wanasema ni maelekezo ya Rais kwamba fedha ziondolewe kwenye fungu hili, zipelekwe wizara hii.”

Vipindi vya Bunge
 Kadhalika, Mbowe alisema uamuzi wa Serikali kuminya uhuru na madaraka ya Bunge umewapora wananchi haki yao ya kupata habari kwa kuzuia mijadala bungeni kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari.

Alisema jambo hilo ni uvunjwaji wa Ibara ya 18 ya Katiba inayotoa uhuru kwa kila mtu kutoa maoni na kueleza fikra zake, kutafuta, kupokea na kutoa habari.

“Bunge ndipo mahali ambapo wananchi wanahoji na kuiwajibisha Serikali na wanajadili hoja za maendeleo kupitia wabunge wao waliowachagua, hivyo huwafuatilia kupitia kwenye luninga zao pia ubadhirifu wa miradi mingi uibuliwa huko,” alisema.

Alisema wapinzani wataendelea kutafakari kwa kina na makini hatua za kufuata na kisha akawasilisha.

“Kwa mazingira kama hayo, kambi rasmi ya upinzani bungeni haiko tayari kuendelea kushiriki katika uvunjaji Katiba, sheria na haki za msingi za wananchi,” alisema.

“Kambi rasmi haitakuwa tayari kuwasilisha hotuba yake katika mazingira haya na inaushauri uongozi wa Bunge kutafuta ufumbuzi wa haraka wa kadhia hii ili kurejesha heshima ya Bunge na haki za msingi.”

Baadaye, Chenge aliipinga kauli ya Mbowe kuwa Katiba imevunjwa na kusema alitumia maneno mazito na badala yake alimtaka atumie maneno kuwa Katiba ilitaka kuvunjwa.

Chenge aliitaka kambi ya upinzani kufuata taratibu kama wanaona kuwa wameonewa, badala ya kutumia maneno hayo na pia akata watafakari kama wangependa kuendelea na mjadala.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walionyesha kususia kwani hata walipoitwa na mwenyekiti hawakuchangia licha ya kuwapo ndani ya ukumbi wa Bunge.

Kauli ya Mbowe kwa wanahabari
Akizungumza na wanahabari Mbowe alisema uamuzi huo haujakiuka sheria kwa sababu Bunge liko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kwamba hawawezi kwenda mahakamani ili kupata tafsiri kuhusu suala hilo kwa sababu shughuli za Bunge zinatatuliwa na Bunge lenyewe si mahakama.

“Rais kama kiongozi wa nchi ana mamlaka ya kulisemea hili, atueleze kama ni yeye ndiye aliyeruhusu Bunge lisirushwe moja kwa moja. Awali walisema TBC hawatarusha ila kwa sasa vyombo vyote vimezuiwa,” alisema.

“Hivi sasa luninga zilizopo ndani ya Bunge zilizokuwa zikionyesha matangazo  nazo hazionyeshi kinachoendelea. Sasa watumishi wa Bunge watafuatilia nini?” alihoji Mbowe.

Kauli ya AG
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema: “Nitashukuru kama mtavuta subira majibu ya Serikali yatatolewa wakati wa kufanya majumuisho.”

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad