Serikali inatarajiwa kuwasilisha miswada mbalimbali ya sheria katika Mkutano wa Bunge la Bajeti utakaloanza kesho mjini Dodoma ili ijadiliwe na kupitishwa na wabunge.
Miswada mingi ya sheria imekuwa ikilalamikiwa na wadau, hata Rais John Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 mwaka jana, alilalamikia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011.
Alisema kuwa sheria hiyo inatoa mianya kwa watumishi kuiba fedha za umma.
Katika mkutano huo, Bunge linatarajia kujadili na kupitisha miswada miwili ambayo ni wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016.
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya jana alisema Serikali itawasilisha pia bungeni miswada mingine ya sheria ijadiliwe na kupitishwa baada ya kupitisha bajeti kukamilika.
Hata hivyo, alisema Bunge bado halijapokea miswada itakayowasilishwa na Serikali zaidi ya hiyo miwili, lakini kuanzia Juni 24 hadi 30 zimetengwa kwa ajili ya kujadili miswada mingineyo.
Mwandumbya alisema pamoja na shughuli hizo, jumla ya maswali 465 yataulizwa na kujibiwa na Serikali bungeni na kila Alhamisi yataulizwa Maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu na anatarajia kujibu jumla ya maswali 88.
“Baada ya wabunge kujadili miswada itakayowasilishwa na Serikali, hoja ya kuahirisha Bunge itatolewa Julai Mosi. Hapo Bunge litakuwa limemaliza kazi yake ya kujadili bajeti za wizara zote katika mkutano huu,” alisema Mwandumbya.