Mtu mmoja ameuawa na tembo wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mapambano kati ya wananchi na kundi la tembo yaliyotokea katika kijiji cha kitendeni kata ya Irkaswa tarafa ya Endyment wilayani Longido mkoa wa Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Longido Bw.Ernest Kahindi amesema katika mapambano hayo pia tembo mmoja ameuawa na wengine sita wamejeruhiwa na kwamba hali katika eneo hilo sio shwari na huenda kukawa na madhara makubwa zaidi.
Akizungumza wakati anaelekea katika eneo la mapambano hayo yanayodaiwa kuanza mapema alfajiri Bw.kahindi amesema hatua za awali za kutuliza hali hiyo zilikuwa zinaendelea kwa ushirikano wa viongozi wa ngazi mbalimbali na watendaji wa idara za wanyamapori zikiwemo za kuwaondoa tembo hao katika eneo hilo zoezi ambalo licha ya kuwa gumu lilikuwa linaendelea vizuri.
Aidha Bw.Kahindi amesema tofauti kati ya tembo hao na wananchi ilijitokeza baada ya wanyama hao kumuua kijana mmoja wa jamii ya kifugaji na ndipo wananchi hao wakajikusanya na kuanza kuwatafuta tembo hao na kuanza kupambana nao kutaka kulipiza kisasi ambapo pia mwananchi mwingine mmoja amejeruhiwa vibaya na tembo zaidi ya sita pia wamejerihiwa vibaya kwa kuchomwa mikuki na kupigwa kwa silaha zingine za jadi.
Hata hivyo Bw.Kahindi ambaye ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuelekea eneo la tukio amesema taarifa kamili ya tukio hilo na hatua zitakazochukuliwa itatolewa baadaye japo ameendelea kuwaomba wananchi kuepuka kuchukua sheria mkononi ikiwemo ya kuamua kupambana na wanyama ili kuepusha madhara zaidi kutokea.
Asilimia kubwa ya eneo hilo ambalo ni mapito ya wanyama kwa muda mrefu sasa limekuwa katika hekaheka kati ya wananchi na wanyama hao hasa unapotekea uharibifu ukiwemo wa wanyama kula mifugo ya wananchi ama kuua watu.