Nani Atashuka Daraja leo Coastal Union Au African Sports..Dakika Tisini Kusubiriwa


Dakika 90 za mchezo wa leo kati ya wapinzani wa jadi Coastal Union vs African Sports zitaamua ni timu gani itaanza kuipa mkono wa kwa heri ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu huu. Timu itakayokubali kichapo ni wazi itakuwa imeiaga ligi huku matokeo ya sare yakiwa mabaya kwa timu zote.

Maandalizi kwa pande zote tayari yamekamilika, African Sports wao wakiwa wamejichimbia maeneo ya Mwakidila wakijifua vikali chini ya kocha wao Athumani Cairo kikosi chao kikiwa kimekamilika bila majeruhi.

Kwa upande wa Coastal Union kocha mkuu Ally Jangalu amesema, vijana wake wako vizuri na wanazidi kuimarika kadiri siku zinavyokwenda mbele.

Mimi ninashukuru kwasababu mpaka sasa hivi tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya African Sports lakini kama sisi tumejiandaa vizuri basi na wapinzani wetu watakuwa wamejiandaa vizuri. Sisi tumejiandaa kushinda na wenzetu wamejiandaa kwa ajili ya kushinda, basi atakaecheza vizuri ashinde kwasababu timu zote ni za nyumbani.

“Kila mchezaji anaelewa matokeo ya sare au kufungwa yanamaanisha sisi ndiyo tumeiaga ligi kuu lakini tangu tumecheza na Simba kiwango chetu kimekwenda juu, tukacheza na JKT Ruvu tukashinda lakini hata mchezo wetu dhidi ya Yanga licha ya kufungwa, uwezo wa Coastal kila mtu kauona”, Ally Jangalu anasema kuelekea mchezo wa leo jioni.

Wakati huohuo mchezaji wa kimataifa wa Coastal Union Chidiebere Abasirim ameutaka uongozi wa klabu hiyo umkabidhi barua yake ya kumsimamisha huku akisisitiza kulipwa mshahara wake.

Chidiebere anaidai Coastal Union mshahara wa miezi mitatu madai ambayo yanatofautiana na kauli ya kaimu katibu mkuu wa Coastal Union Salim Bawazir kwamba wamemsimamisha nyota huyo na wanaendelea kumlipa mshahara wake.

“Chidiebere tumemsimamisha kwa michezo mitatu na tunaendelea kumlipa mshahara wake, bado ni mchezaji wetu halali na ataendelea kulipwa mshahara wake kama kawaida”, anasema Salim Bawazir.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. MAMBO AFRICAN SPORT BANA,COASTAL TUPA KULE.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad