ALIYEKUWA kocha wa Chelsea kabla ya kutimuliwa, Jose Mourinho amekuwa akihusishwa kuhamia klabu ya Manchester United msimu ujao huku taarifa za wazi zikisema kuwa tayari ameshasaini mkataba wa awali wa kukinoa kikosi hicho cha Mashetani Wekundu.
Ripoti kutoka kwenye redio ya Cadena Cope ya nchini Hispania zinasema kuwa kandarasi ya Mreno huyo kuhamia Man U imeleta sintofahamu baada ya wamiliki wa klabu hiyo (Familia ya Glazer) kumgomea kujiunga na Man U.
Kocha huyo mahiri duniani mwenye umri wa miaka 52 amekuwa na matumaini makubwa ya kuinoa Man U msimu ujao ili kumrithi Louis van Gaal anayeonekana kushindwa kuimudu klabu hiyo na kufikia malengo yake.
Mourinho aliyewahi kuifundisha Real Madrid alitimuliwa Chelsea mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza na nafasi yake kuchukuliwa na Guus Hiddink kwa muda kabla ya jana kumteua rasmi Antonio Conte kuwa kocha wao Mkuu.
Kwa upande wake Mwenyekiti Msaidizi wa Man United, Ed Woodward amesema, Van Gaal anamkataba wa miaka mitatu klabuni hapo, lakini wapo tayari kumpa muda wa miaka miwili tu kuendelea kuinoa klabu hiyo na endapo atashindwa kuisaidia kunyakuwa Kombe la Mabingwa (Champions League) basi atalazimika kuondoka klabuni hapo.
Japo ndani ya Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Manchester United kutofautiana mitazamo kuhusu nani ainoe klabu yao msimu ujao, Ed Woodward ndiyo mwenye maamuzi ya mwisho iwapo ni Mourinho au Van Gaal kuinoa hiyo msimu ujao.