Jeshi la Polisi linawashikilia vijana zaidi ya 18 wenye umri kati ya miaka 14 na 20 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu katika maeneo ya Wilaya ya Temeke.
Kamanda wa polisi wa Temeke, Gilles Muroto amesema leo kuwa vijana hao, wanaohusishwa na kundi la Panya Road linalofanya unyang'anyi maeneo ya jiji la Dar es Salaam, walikamatwa jana nyakati tofauti baada ya polisi kuendesha msako wa kuzuia na kupambana na wahalifu.
Alisema vijana hao wanatoka maeneo ya Buza Kanisani, Chanika, Yombo Kirakala, Buza Changulu, Yombo Makangawe na moja anayeishi maeneo ya Mwananyamala lakini alikamatwa Temeke.
"Kama Kamanda Simon Sirro alivyosema kuwa ni lazima wahalifu wadhibitiwe katika mko huu. Temeke hatuwez kumwangusha, tunatekeleza agizo lake,"alisema Kamanda Muroto.
Alisema vijana hao wanajihusisha na vitendo vya uporaji wa mali mbalimbali kuanzia mitaani, pia kujeruhi watu hali inayosababisha wakazi wa eneo husika kuishi kwa hofu.
Alisema upelelezi ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Wakati huohuo, Kamanda Muroto amesema polisi inashikilia mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa Buza baada ya kumkuta na puli 120 za dawa za kulevya aina ya bangi.