Polisi Wakwama Kuuwasilisha Mkataba wa Lugumi.....Wabunge Watoa Siku 3 Mkataba Huo Upelekwe

BUNGE limetoa siku tatu kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mkataba wa Kampuni Lugumi Enterprises wenye thamani ya Sh bilioni 37.

Hatua hii inakuja siku mbili baada ya jeshi hilo kudaiwa kukaidi agizo la kamati hiyo, iliyotaka likabidhi nyaraka za utekelezaji wa mkataba ufanyiwe tathmini kutokana na malalamiko yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) katika hesabu za mwaka 2013/2014.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshi Hilaly alisema agizo la kamati la kutaka mkataba huo, lilitolewa wiki iliyopita kuwezesha wabunge kuangalia utekelezaji wake.

“Jana (juzi) ilikuwa siku ya mwisho kwa jeshi kuwasilisha mkataba huo ofisi za Bunge, lakini mpaka leo (jana) muda huu ninapozungumza nanyi (saa 7:30 mchana) walikuwa hawajawasilisha. “

"Siku zote tumekuwa tukitoa maagizo kwa mdomo na taasisi nyingi zimekuwa zikitekeleza, lakini hili la mkataba wa Lugumi naona kwa wenzetu limekuwa gumu, hivyo tumeamua kuwakumbusha kwa maandishi,” alisema.

Alisema kamati hiyo imetoa siku tatu tangu barua itakapopelekwa na ofisi za Bunge, kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kamati hiyo iweze kupitia utekelezaji wa mkataba huo na baadaye kupeleka mapendekezo kwenye Bunge.

“ Katika suala hili, Kamati haitarudi nyuma, hivyo tunawaomba wenzetu wa Jeshi la Polisi kutupa ushirikiano, si jambo la peke yangu kuamua, ni la Bunge, baada ya kupitia tunapeleka mapendekezo bungeni ambalo ndilo litakaloamua nini kifanyike,” alisisitiza.

Kamati ya PAC ilipokuwa ikipitia hesabu za Jeshi la Polisi, ilibaini kuwapo mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises .

Kupitia mkataba huo wa mwaka 2011, Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Inadaiwa kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37 ikiwa ni sawa na asilimia 99 ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine katika vituo 14 pekee katika jiji la Dar es Salaam, ambavyo pia inadaiwa havijulikani maeneo vilipo.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ukisikia jipu ndio hilo sasa!!! haya bwana wakubwa wanafaidi.

    ReplyDelete
  2. kuna watu sijui wapo juu ya sheria nchi hii ama nini maana mm sielewi......kwa nn wanakaidi agizo la bunge kupeleka mkataba na nyaraka zingine.kutii sheria bils shuruti ni kwa raia tu wao ndo wapo juu ya sheria ama nini???Hapa raisi akifumbia macho tunajua ni muonevu na anaonea vidagaa tu samaki anaziogopa.......na atapoteza credibility kwa wanzania

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad