Kilio hicho kilikuwa ni kufanyia kazi taarifa na mapendekezo mbalimbali dhidi ya ufisadi, usimamizi mbovu, ukiukwaji kanuni na malipo ya wafanyakazi hewa, lakini hakikuwa kikifanyiwa kazi hadi baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani.
Rais John Magufuli sasa ameanza kupekua mafaili aliyoyakuta mezani yanayofichua ufisadi na kupendekeza njia bora ya kudhibiti, akifanyia kazi kwa kutumbua majipu na kuweka kwenye mkakati mapendekezo hayo, hasa yaliyotolewa na CAG.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini hatua zilizochukuliwa na Serikali ya JPM ni matokeo ya kufanyia kazi mapendekezo yaliyomo katika ripoti za CAG za kuanzia mwaka 2009/ 2010 na 2013/ 2014 ambazo zilitolewa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Ripoti hizo zinapendekeza namna bora ya kuongeza vyanzo vya mapato pamoja, kudhibiti na kuratibu matumizi ya fedha, likiwamo suala la upunguzaji wa mishahara ambalo limeibua mjadala tangu Rais Magufuli alipolitamka wakati akiwa mapumzikoni Chato mkoani Geita.
Ripoti hizo zilikuwa zikifanyiwa kazi nusunusu au kwa shinikizo la Bunge la Jamhuri ya Muungano, kiasi cha CAG kuonekana kama anakata tamaa.
“Ninapenda kuifahamisha Serikali kwamba, mapendekezo ninayoyatoa mara kwa mara yana lengo la kuhakikisha kunakuwa na hatua madhubuti na umakini katika kuimarisha ukusanyaji na utumiaji wa mapato na rasilimali za Taifa,” anasema CAGk katika ripoti ya mwaka 2013/ 2014.
“Mapendekezo hayo pia yanalenga kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaidhinishwa na wenye mamlaka na fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Kwa hali hiyo, kwa kuzingatia sheria na kanuni katika kutumia rasilimali za Taifa; thamani ya fedha, tija na ufanisi vyaweza kufikiwa.
“Kwa misingi hiyo, ninaona ni vyema kuyarudia tena mapendekezo niliyoyatoa katika ripoti zilizopita ambayo hayajatekelezwa au yametekelezwa kwa kiwango kidogo na Serikali, Bunge, bodi za wakurugenzi na watendaji wakuu wa mashirika ya umma.”
Baadhi ya mapendekezo ya CAG ambayo hayakuwahi kufanyiwa kazi ni kuweka usawa katika marupurupu yatolewayo na mashirika na taasisi nyingine za umma, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutumia mita za kupima mafuta zilizotelekezwa, kufuatilia misamaha ya kodi, pamoja na kuhimiza matumizi ya mashine za elektroniki.
Mapendekezo hayo na mengine mengi yamefanyiwa kazi kikamilifu na Serikali ya JPM katika kipindi kifupi na kufanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha.
Ripoti ya mwaka 2009/ 2010 na hata ya mwaka 2013/ 2014, inaonyesha CAG alipendekeza uwepo usawa katika marupurupu yatolewayo na mashirika na taasisi nyingine za umma.
“Kuna umuhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa kuna uwiano katika marupurupu wanayopata menejimenti na bodi za wakurugenzi wa mashirika na taasisi nyinginezo za umma, kutokana na ukweli kwamba rasilimali wanazotumia (kama posho za vikao, ada za bodi za wakurugenzi) ni rasilimali za Umma. Hii itasaidia kuondoa tofauti zilizopo sasa, kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika mashirika na taasisi nyingine za umma,” alisema.Pendekezo hilo halikufanyiwa kazi, lakini hivi karibuni Rais Magufuli akiwa Chato, Geita alitangaza kurekebisha mishahara ya wafanyakazi, akisema atapunguza mishahara ya wakurugenzi wa taasisi za umma wanaolipwa hadi Sh40 milioni.
“Katika Serikali ninayoongoza, sitegemei kumlipa mtumishi zaidi ya Sh15 milioni. Tayari nimeunda tume kushughulikia hilo,” alisema Rais Magufuli ambaye amejikita katika kusimamia makusanyo ya mapato, huku akidhibiti matumizi na kupambana na wezi wa mali ya umma.Katika ripoti ya mwaka 2012/2013, CAG alishauri mita za kupima mafuta zilizofungwa na TPA zianze kufanya kazi ili upimaji mafuta yanayoingia nchini ufanywe kwa usahihi.
“Mita hizo ziliwekwa tayari kwa matumizi kwenye bandari za Tanga na Dar es Salaam kwa ajili ya kusaidia kudhibiti mapato yanayopotea kutokana na kutokuwa na vifaa vizuri vya kupimia shehena za mafuta zinazoingia nchini… Hata hivyo, mita hizo zimetelekezwa kwa miaka kadhaa sasa,” anasema CAG.
CAG alisikitishwa na hali hiyo kwa sababu kutotumia vipimo hivyo sahihi na badala yake kupima kwa kutumia kijiti, kulisababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
Lakini Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo alidai vifaa hivyo havikidhi viwango vinavyotakiwa.
“Baada ya matatizo hayo kushindikana, mamlaka ikaamua kuendelea kutumia njia zisizo za kielektroniki (fimbo ya kutumbukiza kwenye matangi ya mafuta) kwenye kupima shehena za mafuta yanayoingia nchini. Kitendo hicho kina athari kwa mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania katika uhakiki wa usahihi wa kiasi cha kodi kinacholipwa kutokana na upimaji wa shehena hizo za mafuta bila ya kutumia vifaa stahiki na athari katika uendeshaji wa shughuli za TPA,” alisema.Februari 11, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea eneo la Kigamboni kukagua ujenzi wa mita hizo kwa ajili ya kupima mafuta yanayoingia ili kujua usahihi wa kiasi cha mafuta yaliyoingia.
Mapendekezo mengine yaliyowahi kutolewa na hayakufanyiwa kazi katika kipindi chote cha utawala wa Rais Kikwete ni kudhibiti misamaha ya kodi.
“Ninapendekeza Serikali iimarishe mfumo wa udhibiti na usimamizi wa misamaha ya kodi inayotolewa na menejimenti ya TRA (Mamlaka ya Kodi Tanzania) iimarishe mfumo wa ukaguzi na uchunguzi kupunguza migogoro kuhusiana na ulipaji wa kodi,” alisema.
“Pia, kuwe na kikao cha kimkakati kujadili maeneo maalumu na njia za kukuza ukusanyaji wa mapato pamoja na kushughulikia rufaa za kesi za kodi nchini. Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoza wafanyabiashara wasiotumia mashine za kielektroniki. Serikali itoe miongozo kwa taasisi zake kuacha kufanya biashara na wazabuni wasiotoa risiti za kielektroniki.”
Katika kipindi chote cha kampeni za urais Magufuli aliahidi kufuta misamaha yote ya kodi isiyo na tija, na baada ya kuingia madarakani siyo tu alitimiza ahadi yake kwa Serikali yake ilianza kufuatilia wote waliotumia vibaya misamaha yakiwamo mashirika ya dini.
Kuhusu ukwepaji kodi Novemba 27 2015 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza TPA ambako ilibainika makontena 349 yamepotea, na siku tano baadaye yaani Desemba 3, 2015 Majaliwa alifanya ziara ya pili ambako alitaja makontena 2431 yaliyopitishwa bila kulipiwa kodi kati ya Machi na Septemba 2014. Serikali iliwataka wahusika wote kulipa kodi huku ikiwasimamisha au kuwafukuza wafanyakazi waliohusika.
Hata suala la kuwaondoa wafanyakazi hewa kutoka kwenye daftari la malipo ni ushauri wa CAG.
“Kuhusu usimamizi wa rasilimali watu na taarifa za mishahara, Serikali inashauriwa kuhakikisha kuwa kasoro hii haitokei na maafisa masuuli wote kuhakikisha mishahara iliyolipwa kwa wasio watumishi wa umma inarudishwa kutoka kwa watumishi hao na kuwasilishwa Hazina,” anasema.Machi 2016 Rais Magufuli alipowateua wakuu wa mikoa na kuwaapisha aliwaagiza kufanya kazi ya kuwaondoa wafanyakazi hewa wote na kuonyesha hakuwa anatania, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela aliyedai hakukuwa na wafanyakazi hewa wakati wapo amefukuzwa kazi.
CAG alipendekeza pia maafisa waliostaafu katika balozi za Tanzania warudishwe nyumbani na nafasi zao kujazwa mara moja. Utekelezaji ulifanyika Januari na Machi wakati balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, pamoja na watumishi wengine watano, waliporejeshwa nchini.
Wengine ni Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Dk James Msekela; na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, Dk Batilda Buriani, baada ya mikataba yao kumalizika.
Wanasiasa walioongea na Mwananchi walipongeza hatua za Rais, lakini baadhi wakata kuwepo na mfumo wa kufanya uamuzi kama huo.
“Rais Magufuli anastahili pongezi kwa hatua alizozichukua kwa kuwa hazikufanywa na mtangulizi wake,” alisema mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini.
“Kuna vitu vingi vinavyoainishwa ndani ya ripoti za CAG na mojawapo ni Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hii imeelezwa mara nyingi kuwa inachangia upotevu wa fedha za Serikali kwa kiasi kikubwa. Kinachotakiwa iondolewe au ifanyiwe marekebisho ili kukabiliana na watu wanaouza bidhaa au huduma zao kwa bei ya juu kuliko ya soko.”Alisema nia nzuri ya Rais kukabiliana na rushwa pamoja na ufisadi itakuwa endelevu endapo kila mtu ataipa kipaumbele wakiwamo wasaidizi wake, lakini akaongeza kuwa jambo hilo linawezekana endapo kutakuwa na kanuni zinazombana kila mtumishi wa umma.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema: “Kama ni ufuatiliaji ni jambo zuri, na mfano mzuri ni hili la watumishi hewa. Tunachotaka kukiona hivi sasa ni hao wanaofanya mpango wa malipo hayo kuchukuliwa hatua.”
Mchungaji Msigwa alisema wapinzani watapata nafasi ya kuzungumzia ufuatiliaji huo wa Rais Magufuli pale watakapoona kuwa wahusika wote wanachukuliwa hatua, akidai sasa kuna maneno mengi kuliko vitendo.
“Mbona hatujaona wakurugenzi wa halmashauri wakichukuliwa hatua maana wao wanajua siri ya mishahara hewa,” alisema.
Kwa upande wake, mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby alisema ofisi ya CAG ni chombo cha Serikali na kinafanya kazi kwa mujibu wa sheria hivyo ni lazima ripoti zake zitekelezwe kwa ajili ya maslahi ya nchi.
“Utekelezaji wa ripoti ya CAG unaipa nguvu ofisi yake lakini pia nashangaa kwa nini mapendekezo yake yalikuwa hayatekelezwi miaka ya nyuma?”Mbunge wa Manyovu (CCM), Albert Obama alisema kila zama zina njia zake za kufuatilia masuala muhimu licha ya kasi ya ufuatiliaji ya Serikali iliyopita ilikuwa ndogo.
“Rais anataka kuleta nidhamu mpya ndani ya nchi kwa kupambana na masuala ya rushwa na ufisadi,” alisema Obama ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji (PIC).
“Nadhani huu ni wakati wa kumpa Rais ushirikiano ili kuweza kubainisha masuala mbalimbali. Hizi ni zama za wanyonge kunufaika na nchi yao.”